1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani imeahidi kusaidia Libya katika maendeleo

Admin.WagnerD9 Januari 2012

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, jana ameahidi kuiunga mkono Libya katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo baada ya kuuondoa utawala wa kimabavu wa Muammar Gaddaf.

https://p.dw.com/p/13gK1
Aussenminister Guido Westerwelle (FDP, M.) kommt am Sonntag (08.01.12) auf dem Flughafen Tripolis-Mitiga in Tripolis (Libyen) an. Westerwelle kam in Tripolis mit Vertretern der libyschen Uebergangsregierung zusammen. (zu dapd-Text) Foto: Thomas Trutschel/Pool/dapd
Westerwelle akiwasili LibyaPicha: dapd

Ikiwa siku ya pili ya ziara yake hiyo, Guido Westerwelle alizungumza na waandishi wa habari mjini Tripoli na kuwahakikisha kwamba nchi yake imesimama imara katika kushirikiana na Libya mpya. Tayari kiongozi huyo amekwishaitembelea Algeria na leo hii anatarajiwa kuwasili nchini Tunisia, kama hitimisho ya ziara yake hiyo.

Miongoni mwa kauli za msingi zilizotolewa na Westerwelle ni kwamba jambo kubwa katika ushirikiano wa Ujerumani na Utawala mpya uliomuondoa Gaddafi ni ushirikiano katika nyanja ya uchumi.

Hata hivyo, aliongeza kusema kwamba Ujerumani itajikita pia katika kusaidia nchi hiyo katika kujenga muundo wa kidemokrasia. Alifanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na waziri mkuu wa Libya, Abdel Rahim al-Keib, na Waziri wa mambo ya nje,  Ashour bin Khayyal.

Ziara fupi ya waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani inaonesha kupungua kwa ushawishi wa nchi hiyo kwa Libya, ikilinganishwa na maeneo mengine ya Afrika ya Kaskazini, na hasa baada ya maamuzi ya kutoshiriki katika kampeni ya mashambulio ya angani ya umoja wa kujihami wa NATO iliouondoa madarakani utawala wa Gaddafi.

Awali akiwa Algeria, katika hotuba yake kuhusu  Libya Westerwelle alizitaja baadhi ya changamoto ambazo libya inakabiliana nazo baada ya miongo kadhaa ya utawala wa kidikteta.

Aussenminister Guido Westerwelle (FDP, l.) steht am Sonntag (08.01.12) in Tripolis (Libyen) waehrend eines Treffens neben dem libyschen Minister fuer Auswaertige Beziehungen, Aschur Bin Chajjal. Westerwelle kam in Tripolis mit Vertretern der libyschen Uebergangsregierung zusammen. (zu dapd-Text) Foto: Thomas Trutschel/Pool/dapd
Westerwelle akiwa LibyaPicha: dapd

Alisema serikali inapaswa kuwapora silaha waasi, kuvijumuisha vikundi vya wanangambo na kuunda jeshi kamili na kufanikisha utawala wa sheria. Hata hivyo, kwa ujumla, kiongozi huyo alisitiza ustawishaji wa demokrasia kwa uwepo wa vyama vingi.

Tangu kuondolewa kwa Gaddafi Ujerumani imekuwa ikionesha nia ya kuisadia Libya kwa njia tofauti na za kijeshi. Zaidi ya watu 1,000 waliojeruhiwa katika mapambano yaliyodumu kwa miezi kadhaa nchini Libya wamepatiwa matibabu katika hospitali za Ujerumani.

Ujerumani pia inaisaidia Libya katika masuala ya ulinzi na kuharibu zana kivita.

Baadae jioni Westerwelle aliondoka nchini Libya kuelekea Tunisia, nchi ambayo vuguvugu la mageuzi kwa nchi za Kiarabu lilianza Desemba 2010. Katika kipindi cha mwezi mmoja tu Watunisia waliweza kumuondoa rais wao. Zine El Abidine Ben Ali, madarakani Januari 14 mwaka jana.

Kiongozi huyo aliyekuwa madarakani kwa takribani miaka 23, hivi sasa anaishi uhamishoni nchini Saudi Arabia.

Katika ziara yake hiyo Westerwelle anatarajiwa kukutana na serikali ya mgawanyo wa madaraka ya nchi hiyo, ambayo imeshika wadhifa baada ya uchaguzi mwaka jana ambao ulikipa ushindi wa kishindo chama cha Kiislamu cha Ennahada.

Vilevile anatarajiwa kukutana na rais mpya wa nchi hiyo, mwanaharakati mkongwe wa haki za binadamu, Monceff Marzouk.

Mwandishi: Sudi Mnette//DPA
Mhariri:  Miraji Othman