Uingereza na Marekani kufanya mazungumzo rasmi | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Uingereza na Marekani kufanya mazungumzo rasmi

Rais wa Marekani George W Bush na Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown wanafanya mazungumzo hii leo kwenye ukumbi wa rais wa kustarehe wa Camp David katika jimbo la Maryland nchini Marekani.Hii ni ziara rasmi ya kwanza ya kiongozi huyo mpya wa Uingereza nchini Marekani.Mazungumzo hayo yanalenga kuupa msukumo mpango wa amani wa eneo la Darfur nchini Sudan aidha kupata kufufua mazungumzo ya biashara ya kimataifa yaliyokwama.Hata hivyo suala la Iraq linatarajiwa kuzungumziwa.

Viongozi wa Uingereza na Marekani katika mazungumzo rasmi huko Camp David

Viongozi wa Uingereza na Marekani katika mazungumzo rasmi huko Camp David

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown alipokewa na wanamaji watatu waliopeperusha bendera ya Marekani na wengine watatu waliopeperusha bendera ya Uingereza.

Hata kabla ya kuwasili kwenye kambi ya jeshi la angani ya Andrews iliyoko nje ya mji wa Washington ,Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown alisisitiza kuwa ziara yake inalenga kuimarisha uhusiano kati ya Uingereza na Marekani.Suala linalojitokeza ni uvamizi wa Iraq.

Kwa mujibu wa Michael Ellam msemaji wa Bwana Brown aliyezungumza na waandishi wa habari mjini London,suala la uvamizi wa Iraq linalounganisha Waziri mkuu wa Uingereza wa zamani Tony Blair na Rais Bush wa Marekani huenda likajadiliwa.Kiongozi huyo anathibitisha kuwa msimamo wa Uingereza haujabadilika kuhusiana na suala hilo.

Kwa mujibu wa ripoti ya tume inayoshughulika na masuala ya Iraq inayoongozwa na Balozi wa Uingereza wa zamani nchini Bosnia Paddy Ashdown,shughuli za kijeshi za Uingereza zinapaswa kusitishwa na majeshi kurejea nyumbani bila kujali hali ya usalama nchini Iraq.

Wakati huohuo Rais Bush anashinikizwa kubadili mikakati yake nchini Iraq japo anashikilia kuwa hatua ya kuongeza majeshi alfu 30 nchini humo huenda ikadhibiti usalama mjini Baghdad.

Kwa upande mwingine huenda Uingereza ikatilia mkazo zaidi shughuli za kijeshi nchini Afghanistan badala ya Iraq.Kwa sasa majeshi alfu 7 ya Uingereza yanahudumu nchini Afghanistan na huenda yakaongezwa hadi alfu 7700 ili kupambana na wapiganaji wa Taleban walio na msimamo mkali.

Bwana Brown anaandamana na Waziri wa mambo ya Nje wa Uingereza David Milliband ambaye alizuru vikosi vya Uingereza nchini Afghansitan pamoja na kiongozi wa nchi hiyo Rais Hamid Karzai.Hiyo ilikuwa ziara yake ya kwanza muhimu katika nchi za kigeni.

Kuhusu suala Darfur Bwana Brown anajaribu kuongeza msukumo wa mpango wa kutafuta amani ya eneo hilo ulioafikiwa wiki jana katika mkutano wa pamoja na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy. Mpango huo unatoa wito wa kupelekwa kikosi kilichoimarishwa cha majeshi alfu 19 ya Umoja wa Mataifa na Afrika , hatua ya kusitishwa kwa vita ,kutekelezwa kwa makubaliano ya amani aidha msaada kwa wakazi wa eneo hilo.

Kuhusu suala la mazungumzo ya kimataifa ya biashara ya WTO Bwana Brown anatoa wito wa kukita katika juhudi za kulegeza masharti ya biashara.Kiongozi huyo alifanya mazungumzo na viongozi wa mataifa ya Brazil,Uchina,India na Afrika Kusini hivi karibuni na kuwashawishi kulipa suala hilo kipa u mbele.Mazungumzo hayo yamekwama kwa sasa.

Waziri Mkuu Gordon Brown anapanga kukutana na viongozi wa vyama vya Republic na Demokratik kabla kuelekea mjini New York kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki- Moon siku ya Jumanne.

 • Tarehe 30.07.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHAL
 • Tarehe 30.07.2007
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHAL

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com