1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhuru wa vyombo vya habari bado tatizo

Source: Reporters without Borders 25 Januari 2012

Shirika la Maripota wasio na Mipaka-RSF-limetoa ripoti yake ya mwaka 2011 inayohusika na uhuru wa vyombo vya habari katika nchi mbali mbali duniani-yaani uwezo wa waandishi habari kufanya kazi bila ya kuingiliwa kati.

https://p.dw.com/p/13pTi
Members of French media watchdog Reporters Without Borders gather near the Iranian embassy in Paris, during a demonstration for press freedom in Iran, Thursday June 18, 2009 in Paris. Two riot policemen are seen standing guard rear center. (ddp images/AP Photo/Francois Mori)
Uhuru wa vyombo vya habari ni changamoto katika nchi nyingiPicha: dapd

Ripoti ya mwaka huu ya RSF, inaonyesha mabadiliko mengi katika orodha ya nchi zilizotajwa, hasa ikizingatia matukio ya mwaka uliopita, yaliyopelekea mageuzi makubwa ya kisiasa, katika ulimwengu wa Kiarabu. Orodha hiyo inadhihirisha uhusiano kati ya demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari. Waandishi habari huripoti juu ya matukio ya uasi kutoka kila pembe ya dunia na serikali za kidikteta hujibu kwa mabavu. Msemaji wa RSF - Michael Rediske anasema, lengo la serikali hizo za kiimla, ni kuzuia habari zote zinazohusika na upinzani - na sio tu kuuzima uasi tangu mwanzoni.


Syria, Bahrain na Yemen zimeanguka sana katika orodha ya mwaka 2011 ulioshuhudia madikteta wengi wa Kiarabu wakitimuliwa madarakani. Eritrea, Korea ya Kaskazini na Turkmenistan zimeshika mkia katika orodha hiyo ya RSF. Katika nchi hizo, raia hawana uhuru wa kueleza maoni yao. Nchi hizo zinafuatwa na Syria, Iran na China, ambako sio waandishi habari tu wanaochukuliwa hatua kali bali hata raia. Mwaka huu, Bahrain pia imewekwa miongoni mwa mataifa yanayokandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Kwa upande mwingine, Finland, Norway na Estonia zinaongoza kwa uhuru wa vyombo vya habari. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, taifa jipya la Sudan ya Kusini lipo katika nafasi ya kuheshimika ya 111 baada ya kujitenga na Sudan inayoshika nafasi ya 170, ikiwa miongoni mwa nchi zenye sifa mbaya kabisa, katika suala la uhuru wa vyombo vya habari.


Uganda, ambako kufuatia uchaguzi wa mwezi Februari, vikosi vya usalama vilitumia nguvu dhidi ya wapinzani na vyombo vya habari, nchi hiyo imeishia nafasi ya 139 baada ya kuanguka kwa nafasi 43. Hata Cote d´Ivoire, iliyoshuhudia umwagaji damu baada ya uchaguzi, imeporomoka kwa nafasi 41 na imeishia nafasi ya 159. Wakati huo huo, kwa mara ya kwanza kabisa nchi mbili za Kiafrika zimo miongoni mwa nchi 20 za mwanzo - hizo ni Namibia na Cape Verde. Mwaka jana, idadi ya waandishi wa habari waliokamatwa, kutekwa nyara au kupigwa wakati wakijaribu kufanya kazi zao, iliongezeka sana.