1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhamisho na usajili wa wachezaji Uingereza

10 Juni 2011

Timu za ligi ya Uingereza zinatumia fedha nyingi kwa wachezaji chipukizi wa nyumbani katika kile kinachoonekana kuwa kuzinduka kwa timu hizo kutokana na ukweli uliopo

https://p.dw.com/p/11YJj
Mshindi wa ligi ya Uingereza msimu uliokwisha, Manchester United.Picha: dapd

Huku kukiwepo sheria ya haki katika malipo kwenye shirikisho la soka Ulaya, UEFA, na mfumo mpya wa kuwalinda kundi maalum la wachezaji, miamba Jordan Henderson na Phil Jones wanatarajiwa kujiunga na Liverpool na Manchester United mtawalia kwa kiasi ya pauni milioni 40.

Ryan Giggs
Ryan Giggs, mchezaji mkongwe wa Manchester unitedPicha: AP

Licha ya kuwa wachezaji wenye majini makubwa pia wanatarajia kusajiliwa kwa msimu unaokuja, shughuli za mapema katika masoko ya uhamisho zinaashiria uwezekano wa mabadiliko ya mtazamo, kama sehemu ya mpango wa muda mrefu.

Kutokana na maonyesho mazuri ya Chris Smalling ya uwezo wake wa kucheza katika kikosi cha kwanza baada ya kusajiliwa kutoka Fulham mwaka uliopita, akiwa na umri wa miaka 20, Manchester United imemlenga sasa Phil Jones, mwenye umri wa miaka 19, kipa wa Atletico Madrid, David de Gea, mwenye umri wa miaka 20, na pengine pia mchezaji wa kiungo cha kati wa Everton, Jack Rodwell.

Wachezaji hawa sio wa bei ya chini, kama ilivyogunduwa Liverpool, ilipolazimika kulipa pauni milioni 35 kumnunuwa Andy Caroll mwenye umri wa miaka 22 mwezi Januari mwaka huu. Hatahivyo, mapato ya baadaye yakizingatiwa mikataba kama hii, huwa na thamani zaidi kuliko kuwasajili wachezaji waliobobea ambao hutaka mishahara mikubwa.

Na pia kutokana na busara ya kibiashara, mchezaji mwenye umri mdogo kama miaka 20 kwa mara nyingi bei yake ya uhamisho, tuseme kwa mfano baada ya miaka mitano, huwa ile ile au hata ikaongezeka.Tofauti na mchezaji mkongwe anayenunuliwa katika mika 28 au 29 na thamani yake huwa inashuka aingiapo katika miaka ya 30.

Mkurugenzi wa Liverpool, Kenny Dalglish, aliwajibika vilivyo msimu uliopita kuwasajili wachezaji wa nyumbani, na hili ni jambo linalotazamiwa kuongezeka katika siku zijazo wakati timu zinajitahidi kuweka hesabu zake za fedha za utumizi na mapato kuwa sawa.

Hapo jana, wenyekiti wa timu 20 za ligi ya Uingereza walikutana kujadili mbinu za kuendeleza mfumo wa mafunzo ya soka, ikiwemo kuanzisha shule za mabweni kwa mafunzo hayo na kuongeza muda wa ukufunzi kwa wachezaji chipukizi.

Fikra ni kuziruhusu timu kuwasajili wachezaji bora chipukizi kwenye shule hizo na kuwezesha kutoa mafunzo zaidi ya soka kwa mujibu wa sheria za taasisi hizo ambazo tayari zimeanzishwa Uhispania, Uholanzi,Brazil na Argentina.

Champion League Inter Milan Barcelona
Mholanzi, Wesley Sneijder wa timu ya Inter MilanPicha: AP

Ufadhili uliopo katika timu ya Manchester United na Chelsea zinaziwezesha timu hizo kuwa katika kiwango tofauti cha uchezaji, na huenda zikawasjili wachezaji wenye majina makubwa kutoka ng'ambo na licha ya kuwa Manchester imehusishwa na mchezaji wa kiungo cha kati wa Inter Milan, Wesley Sneijder, pia inamtaka mfungaji wa Aston Villa anayetoka Uingereza, Ashley Young.

Na hili wengi wanasema linatia moyo kuziona timu za Uingereza zikitazama mustakabali wake kwa kuwasajili wachezaji wadogo walio na uzoefu kwenye ligi ya Uingereza.

Mwandishi:Maryam Abdalla/Rtre
Mhariri:Miraji Othman