1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Ufilipino yajitolea kuiongoza ASEAN badala ya Myanmar

5 Septemba 2023

Ufilipino imejitolea kuchukua nafasi ya uenyekiti wa zamu wa jumuiya ya nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia ASEAN, badala ya Myanmar iliopangwa kuchukuwa wadhifa huo mnamo 2026.

https://p.dw.com/p/4Vz7c
Indonesia I Mkutano wa kilele wa ASEAN
Waziri wa mambo ya nje wa Indonesia Retno Marsudi, kulia, akimsalimia waziri wa mambo ya nje wa Singapore Vivian Balakrishnan, baada ya kuwasili Jakarta, Septemba 4, 2023. Picha: Dita Alangkara/AP Photo/picture alliance

Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr alitangaza uamuzi huo katika mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo unaoendelea mjini Jakarta, wakati Jumuiya hiyo kipambana na jinsi ya kushirikiana na watawala wa kijeshi wa nchini Myanmar.

Amesema uamuzi huo unalenga kuimarisha jumuiya hiyo ya ASEAN wakati inapoanza ukurasa mwingine. Hata hivyo wanadiplomasia wawili ambao hawakutaka kufahamika wamewaambia waandishi wa habari kwamba, hatua hiyo iliafikiwa na viongozi wa jumuiya baada ya kuiomba Ufilipino kuchukua hatamu.

Soma pia:Indonesia yahimiza suluhisho la kisiasa Myanmar 

Msemaji wa utawala wa kijeshi myanmar Zaw Min Tun amelithibitishia shirika la habari la AFP kwamba nchi yake haitachukua uenyekiti wa ASEAN mnamo 2026 japo hakufafanua  zaidi. Kwa upande mwingine  rais Ferdinard Marco wa Ufilipino nae hakusema kwanini Manila imeridhia uenyekiti huo wa jumuiya.

Kuendelea kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Myanmar, kuzuka kwa mizozo na machafuko ya muda mrefu yanayoendelea katika eneo la Bahari ya kusini mwa China ni miongoni mwa ajenda muhimu zilizogubika mkutano huo wa  jumuiya hiyo yenye nchi wananchama kumi.

Indonesia ASEAN
Ufilipino itachukuwa uenyekiti wa mzunguko wa jumuiya ya ASEAN mwaka 2026 katika pigo kwa utawala wa kijeshi wa Myanmar, unapambana kutambuliwa kimataifa baada ya mapinduzi ya 2021.Picha: Mast Irham/AP Photo/picture alliance

Kando na hayo masuala yenye utata ikiwa ni pamoja na ushindani wa Marekani na China katika eneo hilo ambao umeleta mgawanyiko wa wazi ndani ya ASEAN.

Uwanja wa ushirikiano badala ya malumbano

"Msigeuze jahazi letu, ASEAN, kama uwanja wa mashindano yanayosababisha uharibifu wa pande zote. Badala yake, tumieni jahazi hili la ASEAN kama uwanja wa ushirikiano, kuunda ustawi, kuunda utulivu, kuunda amani, sio tu kwa eneo bali kwa ulimwengu," alisema rais wa Indonesia Joko Widodo, mwenyeji wa mkutano wa ASEAN.

ASEAN imewapiga marufuku viongozi wa kijeshi wa Myanmar kushiriki katika mikutano yake ya ngazi za juu lakini tofauti zimeibuka huku Indonesia ikijaribu kushirikisha pande zote kushinikiza mpango wa amani wa ASEAN na Thailand kujaribu kuwashirikisha viongozi wa kijeshi wa Myanmar.

Soma pia:Mataifa ya ASEAN yaunda rasmi jumuiya 

ASEAN iliafikiaana juu ya mpango wa amani, unaojulikana kama makubaliano yake yenye vipengele vitano, ambayo yanataka kukomesha ghasia na kufanyika mazungumzo kati ya vyama vyote, lakini majenerali hawajazingatia kwa umakini mpango huo.

Indonesia ASEAN
Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya ASEAN waliokutana nchini Indonesia, Septemba 4, 2023.Picha: Mast Irham/AP Photo/picture alliance

Kulingana na Umoja wa msaada kwa wafungwa wa kisiasa,na wafuatiliaji wa masuala ya haki za binadamu, vikosi vya usalama vya Myanmar vimewaua takriban raia 4,000 na waliwakamata wengine 24,410 tangu jeshi lichukue mamlaka.

Mapinduzi ya mapema ya 2021 yalizima harakati za kidemokrasia na kumaliza muongo mmoja wa mageuzi ya muda, ikiwa ni pamoja na chaguzi mbili alizoshinda mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi, na kurudisha nyuma matumaini katika ASEAN na kwingineko kwamba, Myanmar ilikuwa inaelekea kwenye serikali ya kiraia, utulivu wa kisiasa na ukuaji wa uchumi.

Chanzo: Mashirika