1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mtoto wa dikteta wa zamani ashinda urais Ufilipino

Mohammed Khelef
10 Mei 2022

Mamia ya watu wameandamana katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila, kupinga matokeo ya awali yanayoonesha kuwa mwana wa dikteta wa zamani, Ferdinand Marcos, anaongoza kwa ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa Jumatatu.

https://p.dw.com/p/4B5D5
Philippinen | Ferdinand "Bongbong" Marcos Jr.
Picha: REUTERS

Wakiwa wamebeba mabango yanayosomeka: "Zuia udanganyifu wa kura", waandamanaji hao wanapinga kile wanachosema ni ukiukwaji wa sheria katika uchaguzi huo wa jana, ambapo maelfu walishindwa kupiga kura zao kutokana na mashine za kupigia kura kutofanya kazi. 

Katika baadhi ya maeneo, wapigakura walisubiri usiku mzima kungojea mashine zitengenezwe, lakini Tume ya Uchaguzi ya Ufilipino ilikataa pendekezo la kuongeza muda wa kupiga kura, ikisema idadi ya mashine zilizoharibika ilikuwa ndogo mno kuweza kuathiri matokeo jumla ya uchaguzi.

Polisi wa kutuliza ghasia walitawanya waandamanaji hao, waliokuwa wakimlaani Ferdinand "Bongbong" Marcos Jr na mgombea mwenza wake, Sara Duterte-Carpio, ambao wanaongoza matokeo ya awali na yasiyo rasmi yaliyotolewa hadi sasa.

Ushindi wa kishindo

Präsidentschaftswahl auf den Philippinen
Wafuasi wa Ferdinand "Bongbong" Marcos Jr. wakishangiria ushindiPicha: Willy Kurniawan/REUTERS

Kwa mujibu wa matokeo ya awali na ambayo bado si rasmi, Ferdinand "Bongbong" Marcos Jr amepata kura milioni 30.87 zinazomuweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kumrithi Rais Rodrigo Duterte, kuliko mtu aliyeshika nafasi ya pili, makamu wa sasa wa rais, Leni Robredo, mwenye kura milioni 14.73.

Mgombea mwenza wa Marcos Jr, Sara Duterte-Carpio, ni binti wa rais wa sasa, Rodrigo Duterte, na anaongoza kwenye uchaguzi wa umakamu wa rais, akiwa na kura milioni 31.30, akifuatiwa na mgombea mwenza wa Robredo, Seneta Francis Pangilinan, mwenye kura milioni 9.173. 

Robredo aliwaasa wafuasi wake kusikiliza kauli ya umma, akisema licha ya kufahamu kuwa kuna ghadhabu zinazotokana na ripoti za mapungufu kwenye uchaguzi huo, hiyo haipaswi kuwa sababu ya machafuko. 

Kurudi kwa kizazi cha madikteta

Präsidentschaftswahl auf den Philippinen
Waandamanaji wakipinga matokeo ya urais ambayo yanampa ushindi Ferdinand "Bongbong" Marcos Jr nchini Ufilipino.Picha: REUTERS

Shirika la haki za binaadamu la Karapatan limesema kwenye taarifa yake kwamba "wawili hao wanawakilisha aina mbaya kabisa ya siasa na utawala wa kikale kwenye historia ya Ufilipino."

Shirika hilo limetowa wito kwa raia kumiminika kwa wingi mitaani kupinga kurejea madarakani kwa kizazi cha watawala wanaotajwa kuwa makatili zaidi kwenye historia ya taifa hilo.

Naye meya wa mji mkuu Manila, Francisco Domagoso, amekubali kushindwa kwenye uchaguzi huo wa jana.

Muigizaji huyo wa zamani aliyefahamika kwa jina la kiusanii la Isko Moreno, alitumia ukurasa wake wa Facebook kuwapongeza washindi akisema anatambuwa matakwa ya wapiga kura.