1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yachukua urais wa Umoja wa Ulaya

Charo, Josephat1 Julai 2008

Katika miezi sita ijayo, Ufaransa itakuwa na kazi kubwa katika kuyashughulikia maswala ya kuyalinda mazingira, sera za kilimo, uhamiaji na ulinzi.

https://p.dw.com/p/EU6n
Rais Nicholas Sarkozy wa UfaransaPicha: AP

Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy anataka kuwasilisha mpango mpya baada ya jamhuri ya Ireland kuukataa mkataba wa Lisbon unaopendekeza mageuzi mapya katika Umoja wa Ulaya. Kuna uwezekano wa kura ya maoni juu ya mkataba wa Lisbon kurudiwa huko Ireland mwanzoni mwa mwezi wa Januari mwaka ujao wa 2009. Rais Sarkozy amedokeza kwamba mkataba mpya wa Umoja wa Ulaya hauhitajiki kwa haraka na nchi wanachama wa umoja huo pekee.

´Ili kuwezesha upanuzi wa Umoja wa Ulaya, tunahitaji mkataba wa Lisbon. Vinginevyo mkataba wa Nizza utaendelea kutekelezwa katika nchi 27 wanachama. Ufaransa inataka mataifa ya Balkan yajiunge na Umoja wa Ulaya, lakini chini ya mkataba wa mageuzi. Nchi wanachama zinazotaka sana umoja huu upanuke, sharti zifahamu kwamba bila shaka tunahitaji taasisi mpya.´

Bila shaka Wafaransa wanataka kuendeleza juhudi za kuidhinishwa kwa mkataba mpya wa mageuzi wa Umoja wa Ulaya, lakini pia watatakiwa kwa uwezo wao wote washughulikie maswala nyeti ya kisiasa kama vile sera za uhamiaji, viwango vya gesi ya carbon inayotoka viwandani na kuimarishwa kwa sera ya pamoja ya ulinzi. Mbali nahayo Ufaransa inataka kufikia lengo la kupunguza kodi ya mafuta ya serikali kwa sababu ya kupanda kwa bei za mafuta.

Katika makao makuu ya Ulaya mjini Brussels viongozi wanazungumzia kujitayarisha kwa urais wa Wafaransa. Halmashauri ya umoja huo na bunge linatarajia mafuriko ya mawazo mapya kutoka kwa Ufaransa. Jacki Davis wa taasisi ya sera za Ulaya mjini Brussels Ubelgiji anasema Umoja wa Ulaya utakuwa tayari kuyapokea mawazo hayo hususan ikizingatiwa mzozo wa mkataba wa Lisbon unaoukabili.

´Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya kila mara hutaka kuendeleza ufanisi mkubwa. Nicholas Sarkozy tayari pengine ni kiongozi anayetazamwa na wengi. Kwa hiyo umoja huo unaweza kuendelea kwa nguvu mpya, lakini lazima kuwe na uwiano kuzingatia jukumu la rais wa umoja huo, ambalo si kusukuma ajenda binafsi, bali ajenda inayoshughulikia maslahi ya Umoja wa Ulaya kwa jumla.´

Swala litakalopewa kipaumbele ni mageuzi ya ruzuku ya kilimo, ambayo kutokana nayo Ufaransa inanufaika sana kwa sasa. Swala hilo litajadiliwa kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya ambapo kunatarajiwa kuw ana mjadala mkali na nchi kama vile Uingereza, ambazo zinataka ruzuku kwa wakulima ipunguzwe.

Urais wa Ufaransa unaanza na mkutano wa kilele katika majuma mawili yajayo ambapo umoja wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia unatakiwa kuzinduliwa. Umoja huu kwa mtazamo wa Ujerumani ni mojawapo ya ndoto kubwa za rais Nicholas Sarkozy inayovuka mpaka wa Umoja wa Ulaya.