1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani - tarehe 11-01-05

RM11 Januari 2005

Mada iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye safu za maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo ni ushindi wa kiongozi wa chama cha Wapaletina, PLO, bwana Mahmud Abbas kuwa raisi mpya wa Wapalestina. Mada nyingine iliyozingatiwa zaidi hii leo ni mzozo wa vyama vya kisiasa kuhusu msaada wa mafuriko unaotolewa na Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CHOk

Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limeandika yafuatayo juu ya ushindi wa Mahmud Abbas:

"Marekani na Umoja wa Ulaya zinakabiliwa sasa na kazi ngumu, kwani ni kwa ushirikiano na umakini wao tu ndiyo wanaweza kufufua mazungumzo ya amani kati ya waisrael na wapalestina. Hata hivyo hakuna matumaini makubwa. Pamoja na kwamba utawala wa rais Bush umeamua sasa kutoa kipaumbele zaidi kwa suala la Mashariki ya kati, uamuzi huu utakuwa bure, kama Marekani itaendelea kupendelea upande mmoja.

Umoja wa Ulaya mpaka sasa umebaki na jukumu dogo la kutoa fedha tu. Katika kipindi cha miezi ijayo, umoja huu lazima ujitahidi kuchukua majukumu mengine muhimu katika eneo hilo."

Kuhusu mada hii, gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:

"Jambo moja tu limebadilika kwenye mzozo wa Mashariki ya Kati: kiongozi mgumu wa zamani Yassier Arafat hatashiriki tena kwenye mazungumzo ya amani. Kifo chake kimeiachia Israel na Marekani mtihani mgumu. Hawa walisema; Arafat peke yake ndiyo kikwazo cha mikakati ya amani. Kwa mantiki hii, wanatakiwa kuthibitisha sasa kuwa, walichosema ni kweli."

Nalo gazeti la WETZLARER ZEITUNG limetoa maoni yafuatayo:

"Kwa kumchagua Mahmud Abbas, wapalestina wamepiga hatua ya mbele kuelekea kwenye amani. Sasa ni zamu ya Scharon. Uamuzi wa kuwaachia huru wafungwa wa Palestina na kuondoa majeshi yake, ni hatua za kwanza zitakazomsaidia kionzozi mpya wa wapalestina kuyashawishi hata makundi mengine kama vile la Hamas kushiriki kwenye mazungumzo ya amani.
Kwa kufanya hivi, Scharon anaimarisha pia nafasi yake kwenye serikali mpya ya mseto."

Tugeukie sasa mada nyingine iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye magazeti ya Ujerumani hii leo, ambayo ni mzozo wa vyama vya kisiasa kuhusiana na msaada wa mafuriko unaotolewa na Ujerumani.

Mhariri wa gazeti la KIELER NACHRICHTEN ameandika:

Serikali inamwona kiongozi wa mkoa wa Lower Saxony kutoka kwenye vyama vya upinzani, bwana CHRISTIAN WULFF, hana huruma. Kwa kutokana na maangamizi makubwa yaliyosababihwa na gharika ya tsunami, mwanzoni vyama vya kisiasa vilionyesha nia ya kuiacha pembeni mada hii kwenye kampeni za chaguzi ndogo. Hivi sasa mambo yamebadilika.
Gazeti la KILER NACHRICHTEN limemalizia kwa kuandika: Mada hii imeanza kupamba moto kwenye kampeni za uchaguzi – ingekuwa maajabu kama wasingefanya hivyo.

Kwa kumalizia udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tuangalie sasa kilichoandikwa kwenye gazeti la RHEIN-NECKER-ZEITUNG:

"Kama usemi wa zamani bado unathaminiwa,"anayesaidia haraka husaidia mara dufu", basi kansela wa Ujerumani na waziri wake wa fedha wanastahili pongezi kwa msaada waliotoa. Mtu anaweza kusema, wamefanikisha jambo hili kwa kutokana na uzoefu wao kwenye mafuriko. Kama ilivyokuwa kwenye maafa ya mafuriko ya mto Elbe nchini Ujerumani, hapo mwaka 2002, kiongozi wa upinzani, Edmund Stoiber ameanza kulalamikia misaada inayotolewa na serikali.

Kwa mara nyingine, wakati wengine wanatoa misaada, yeye anataka kuanza kuhakiki misaada inayotolewa. Kwa kufanya hivi anaonyesha hapendi kutoa. Kwa bahati mbaya, anafanya hivi kwenye kipindi ambacho mtu hatakiwi kuonyesha ubahili.