1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa China wachupa mipaka na kuzusha wasiwasi

19 Julai 2007

Uchumi wa China umekuwa kwa kasi kubwa kabisa kwa zaidi ya muongo mmoja katika kipindi cha pili cha mwaka.

https://p.dw.com/p/CHk6
Bidhaa za China
Bidhaa za ChinaPicha: AP

Wananchi wa umma wa China wanatarajia serikali huenda ikachukua hatua za haraka kuzuia kustawi kupita kiasi kwa uchumi.

Gharama ya maisha ikipanda kwa kiwango kikubwa nchini China uchumi wan chi hiyo umekuwa kwa haraka zaidi kuliko ilivyotarajia kwa asilimia 11.9 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka na asilimia 11.5 katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa mwaka.

Idara ya serikali ya takwimu za biashara nchini China NBS inasema kwa sasa pato jumla la taifa hilo inatarajiwa kuipiku Ujerumani kama nchi ya tatu kubwa duniani ifikiapo mwishoni mwa mwaka huu ikiwa tayari imeshaipita Uingereza na Ufaransa mwaka 2005.

Hata hivyo pamoja na kuipiku Ujerumani maafisa na wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema serikali ya China huenda ikafikiria zaidi kuhakikisha kasi ya uchumi inapungua kutoka kasi hii ambayo haijawahi kuonekana tangu miaka ya 90’s.

Mara ya mwisho ambapo uchumi wa China ulikaribia kasi hii mpya ilikuwa mwaka 1994 ambapo pato jumla la nchi liligonga asilimia 13.1.

Msemaji wa idara ya NBS Li Xiaochao amewaambia wanandishi wa habari kwamba hatua za serikali zilizochukuliwa kudhibiti kasi ya uchumi ikiwa ni pamoja na kupandisha mara mbili mwaka huu kiwango cha riba zimeanza kuzaa matunda lakini serikali inahitaji kuchukua hatua zaidi.

Aidha msemaji huyo amedokeza kuwa bado yapo matatizo kadhaa yaliyosalia juu ya uchumi wa China nayo ni pamoja na kutokuwepo urari wa biashara,mfumko wa bidhaa za chakula na shinikizo katika masuala ya kuhifadhi nishati na kupunguza uharibifu wa hali ya hewa.

Wiki iliyopita China ilitangaza kwamba katika kipindi cha miezi ya mwanzo wa mwaka pato la ziada la biashara lilifikia hadi dolla billioni 112.5 .

Kinachotia wasiwasi hasa katika uchumi wa China ni mfumko wa bei ambao umepanda kutoka asilimia 3.2 katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa mwaka hadi asimilia 4.4 katika mwezi wa juni kutoka asimilia 3.4 mwezi Mei.

Kiwango hicho kimepita kile cha asilimia 3.0 kinachotarajiwa kwa mwaka na serikali.

Viwanda pia nchini humo vimezidisha uzalishaji wake na kufikia hadi asilimia 25.9 katika nusu ya mwanzo ya mwaka.

Li Huiyong mwanauchumi katika kampuni moja kubwa huko Shangai China anasema dalili zote zinaonyesha kuwa uchumi wa taifa unaelekea kustawi kupita kiasi na serikali italazimika kuchukua hatua kabambe za kuzuia hali hiyo.

Li nawanauchumi wengine wanasema hatua mojawapo muhimu ambayo yumkini ikatangazwa hivi karibuni na serikali ni kupandishwa kwa mara ya tau mwaka huu kiwango cha riba ili kukabiliana na hali ilivyo.