1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin15 Februari 2007

Magazeti ya Ujerumani leo hii hasa yamejishughulisha na ripoti kuwa ukarabati utakaofanywa katika kampuni la gari Daimler- Chrysler ambalo ni mali ya Ujerumani na Marekani, utahatarisha kama nafasi 13,000 za kazi.

https://p.dw.com/p/CHTh

Yafuatayo ni maoni ya magazeti mbali mbali ya Ujerumani.

Kwa maoni ya gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG,uamuzi uliopitishwa na DaimlerChrysler ni mchungu kweli. Kinachohamakisha hapo ni ukiritimba uliokuwepo pamoja na hamu ya baadhi kubwa ya wakurugenzi ya kutaka kupandisha hadhi zao na wapo tayari kwenda umbali wa kubahatisha kufanya mabadiliko.Lakini hakuna maana ya kufanya mabadiliko kwa sababu tu ya kutaka kujaribu kingine-huo ni ukweli uliodhirishwa hapo awali.

Fikra kama hiyo imeelezwa pia na gazeti la FULDAER ZEITUNG.Linasema:

“Kwa hivi sasa mafanikio katika viwanda vya magari ni wa muda mfupi tu.Hata mwenyekiti wa DaimlerChrysler bwana Dieter Zetsche anaefurahiwa kama mwokozi wa Chrysler,safari hii amebanwa vibaya. Kwani ni dhahiri kuwa mpango wa ukarabati alioutangaza hauwezi kuendelea milele.

STUTTGARTER ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

“Ikiwa ni takriban mwongo mmoja tu tangu Daimler-Benz ya Ujerumani na Chrysler ya Marekani kuungana,furaha ya wakuu wa muungano huo imetoweka na ukweli halisi unawatazama machoni kuwa muungano huo haukuleta kile kilichotazamiwa yaani kuwa kampuni lenye nguvu kubwa.Hata kampuni la magari la Kijerumani BMW lilipata somo hilo baada ya kulinunua kampuni la kutengeneza magari la Uingereza,Rover.Kampuni la BMW lililazimika kulipa pesa nyingi mno kwa somo hilo:yaani kuhifadhi tabaka ya juu ya magari na kutengeneza magari kwa wingi ni mambo mawili yasiokwenda sambamba.

Kwa upande mwingine BERLINER ZEITUNG linaeleza kuwa kuna matokeo mengine pia mbali na kupoteza nafasi za ajira zipatazo 13,000.Likiendelea linaonya:

“Litakuwa jambo la busara ikiwa mwenyekiti wa DaimlerChrysler,Dieter Zetsche hatoelemea upande wa tamaa ya masoko ya mitaji.Kwani hatua ya kutengana na Chrysler itasababisha gharama za kutisha.Kwa mujibu wa benki moja,hatua hiyo italigharimu kampuni la Kijerumani Daimler-Benz kama Euro bilioni 26.”

Mada nyingine iliyogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani ni ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto duniani UNICEF.Ripoti hiyo,ni matokeo ya uchunguzi uliofanywa kulinganisha hali za watoto katika nchi za viwanda barani Ulaya.Ujerumani imechukua nafasi ya kumi na moja na hivyo ipo katikati. BERLINER MORGENPOST linasema:

“Ripoti ya UNICEF imetufungua macho kama ile ripoti ya PISA kuhusu shule mbali mbali barani Ulaya.Kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF hali na mustakabali wa watoto katika majimbo ya Bayer,Baden-Württemberg na Hessen huvutia zaidi kulinganishwa na watoto wanaoishi katika majimbo ya Berlin,Sachsen-Anhalt,Mecklenburg-Vorpommern na Bremen.Kinachoshtua zaidi ni kuwa zaidi ya nusu ya watoto wa Kijerumani wenye umri wa miaka 15 waliouhojiwa,walisema kuwa wazazi,mara nyingi hawana hata nafasi ya kuzungumza nao.Matokeo yake ni maafa makubwa-hali ambayo yadhihirika katika jiji la Berlin,lamalizia BERLINER MORGENPOST.