Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 06.03.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii wameshughulikia juhudi za Ujerumani,inayotaka iwepo sera moja ya Umoja wa Ulaya,kuhusu suala la mazingira.

Mada nyingine ni mtazamo mpya wa China kwamba mazingira yanapasa kuhifadhiwa zaidi.Prema Martin na udondozi wa magazeti ya Ujerumani.

Tunaanza na gazeti la TAGESSPIEGEL linalosema:

„Mtazamo huo mpya wa China hauhusiki kabisa na ujamaa.China inaongozwa na kundi dogo la watu wenye elimu ya tabaka ya juu kabisa na hushauriwa na wataalamu.Vile vile tatizo si kwamba serikali inafuata sera isio barabara,kwani siasa zake katika sekta za fedha na viwanda zinaonyesha mafanikio.Kosa lipo katika mfumo wa uongozi.Kwani tangu muda mrefu,jumuiya ya China ina tabaka mbali mbali kwa hivyo ni vigumu kuongozwa kutoka juu kama ilivyokuwa hapo zamani.“

Kwa maoni ya gazeti la HANDELSBLATT China imebadilika sana.Likiendelea linasema:

Warithi wa mwasisi wa taifa hilo,Mao Tse-tung wametupilia mbali mifumo ya kiuchumi ya Marx na Lenin.Siku hizi si aibu tena kuwa tajiri bali hicho ndio kinachotakiwa.Lakini uhuru mpya uliopatikana unaishia kule kule,yaani kwenye chama cha kikomunisti kinachohofia kupoteza mamlaka yake.Hakuna ishara yo yote ile ya haki - ambao ni msingi wa masoko ya uchumi ya kijamii.“

Kwa upande mwingine FINANCIAL TIMES la Ujerumani likieleza maoni yake kuhusu mtazamo mpya wa China linasema:

China inakuwa kijani!Baada ya uchumi wa nchi hiyo kuendelezwa kwa kasi kubwa,bila ya kujali mazingira,sasa Waziri Mkuu Wen Jiabao ametoa ishara dhahiri.Jinsi mada ya ulinzi wa mazingira ilivyopewa umuhimu,mtu anaweza kuamini kuwa serikali safari hii kweli imetia maanani suala la kuhifadhi mazingira.Lakini hata hivyo,China bado haijafika umbali wa kushiriki moja kwa moja kwa vitendo kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Tukigeukia mada nyingine,gazeti la EXPRESS mjini Cologne linasema si rahisi hivyo,kutekeleza mapendekezo ya kuhifadhi mazingira,yaliotolewa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.Hapo subira kubwa itahitajiwa kuweza kukabiliana na vigogo vya mashirika makubwa ya kibiashara.Lakini safari hii,watu wametia maanani zaidi,maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa duniani,kwani wanajadiliana kwa dhati kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.Kwa mfano,asilimia 76 ya wakazi wa nchi za Umoja wa Ulaya,wanataka kupunguza matumizi yao ya nishati.Kwa hivyo,sasa kote duniani,viongozi washinikizwe zaidi kuchukua hatua,kwani wao ndio wenye mamlaka ya kuamua, lamalizia gazeti la EXPRESS.