1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuhuma za Bush dhidi ya Iran zinazusha wasi wasi

P.Martin2 Februari 2007

Wabunge wa Marekani wanajaribu kupunguza uwezo wa rais George W.Bush kuishambulia Iran.

https://p.dw.com/p/CHKq
Rais George W.Bush akihotubia Bunge
Rais George W.Bush akihotubia BungePicha: AP

Wabunge hao wameingiwa na wasi wasi kwa sababu ya matamshi ya baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu serikalini na hata rais George W.Bush,dhidi ya Iran.

Kimsingi,baadhi kubwa ya maazimio yaliopitishwa na wabunge wa Marekani hayana uzito wa kutimizwa. Maazimio hayo yamepitishwa katika Baraza la Wawakilishi na Seneti,yakisisitiza kuwa rais George W.Bush lazima apate idhini ya Bunge kabla ya kufanya shambulio lo lote dhidi ya Iran au nchi zingine zilizo jirani na Irak.

Kwa mfano,azimio jipya lililopitishwa siku ya Jumatano na wabunge watano wa chama cha Demokrats,linasema ni siasa ya Marekani kutojitanguliza vitani na Iran kama hatua ya kujikinga.Vile vile azimio hilo linapiga marufuku kutumia pesa zilizoidhinishwa na Bunge,kutekeleza mipango ya siri yenye azma ya kubadilisha serikali au kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Tehran,ikiwa hakuna kitisho cha hapo hapo.

Wabunge wengi katika Baraza la Seneti,wameiuliza serikali ya Bush ikiwa inaamini,ina mamlaka ya kikatiba,kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya Iran bila ya idhini ya Bunge.Ukweli kwamba serikali bado haijatoa jawabu rasmi kwa masuala kama hayo,haukuchochea tu khofu bungeni na kwengineko kuwa Ikulu inaamini jawabu ni “ndio” bali inapanga pia kuishambulia Iran hivi karibuni.

Khofu hizo zimeongezeka juma hili,baada ya maafisa wa kijeshi wa ngazi ya juu kutoa madai mapya kuwa Iran inawapatia wanamgambo wa madhehebu ya Kishia nchini Irak,misaada ya silaha mbali mbali kama miripuko inayopenyeza magari yenye mabamba ya vyuma,hadi makombora ya Katyusha sawa na yale yaliotumiwa na wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon dhidi ya Israel katika vita vya mwaka jana.Makombora hayo lakini bado hayajawahi kutumiwa nchini Irak.

Hata hivyo,baadhi ya watazamaji,tangu muda mrefu wanaamini kuwa Bush ana azma ya kushambulia vituo vya kinuklia vya Iran kabla ya kumaliza miaka yake miwili iliyobaki,kama suluhisho la kidiplomasia halitopatikana kuhusu madai ya Marekani kwamba Iran isitishe mradi wake wa kurutubisha madini ya uranium.Lakini Bunge la Marekani lilizidi kuwa na wasi wasi,baada ya Bush kutoa hotuba yake tarehe 10 Januari kueleza mkakati mpya kuhusu Irak.Katika hotuba hiyo,Bush alizituhumu Iran na Syria kuwa zinawaruhusu magaidi na wanamgambo kuingia na kutoka Irak kwa kupitia nchi hizo mbili.Hasa aliituhumu Iran kuwa inatoa msaada wa silaha kuvishambulia vikosi vya Kimarekani.Kwa hivyo,akatangaza kuwa anatuma manowari ya pili inayobeba ndege za kijeshi, katika eneo la Ghuba.Vile vile aliahidi kuwa atateketeza mtandao unaotoa mafunzo na silaha za kisasa kwa maadui,nchini Irak.

Tangu hapo,Bunge la Marekani limezidi kupokea miswada ya maazimio yenye azma ya kuiongoza serikali,ili ifuate njia isiyochochea mapambano.