Trump atangaza kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel
7 Desemba 2017Kufuatia tangazo hilo la Trump ubalozi wa Marekani sasa utahamishwa kutoka mjini Tel Aviv na kupelekwa Jerusalem.
Akizungumza hapo jana Jumatano katika ikulu ya Marekani White House Trump alisema ni muda muafaka sasa kuitambua rasmi Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kuongeza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kutambua ukweli uliopo kuhusiana na suala hilo.
Licha ya kuonywa mara kadhaa dhidi ya hatua hiyo na viongozi wa mataifa ya kiarabu pamoja na viongozi wa ulaya , Trump amesema anaelekeza serikali yake kuanza matayarisho ya kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv na kuupeleka Jerusalem. Amesema anafanya hivyo kwa kuzingatia sheria ya mwaka 1995 inayoelekeza Marekani kuhamishia ubalozi wake Jerusalem.
Amesema wakati alipoingia madarakani aliahidi kuangalia kwa makini changamoto zinazoikabili dunia na kuwa hauwezi kutafuta suluhisho la matatizo kwa kutumia njia zilezile zilizoshindwa wakati uliopita na kuongeza kuwa changamoto zozote zinahitaji mtizamo mpya.
Aidha Trump ameongeza kuwa wakati marais waliopita walilifanya suala hilo kama ahadi kubwa kwenye kampeni zao lakini walishindwa kutekeleza ila kwa upande wake sasa anatekeleza.
Akizungumzia uamuzi huo wa Trump Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema tangu siku ya kwanza kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa akipinga hatua zozote zinazoweza kuvuruga mchakato wa kuleta amani kati ya Israel na Palestina na kuwa suala linalohusu Jerusalem linapaswa kujadiliwa kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande zote mbili za Israel na Palestina kwa kuzingatia maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na hakuna mpango mbadala zaidi ya suluhisho la mataifa mawili.
Kwa upande wake rais wa Mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas amesema kwa tangazo hilo la Trump Marekani sasa inaonekana imejiondoa katika juhudi za kutafuta amani ya Israel na Palestina ambazo imekuwa ikizisimamia . Katika hotuba yake alioitoa kwa njia ya Televisheni Abbas amesema uamuzi huu wa Trump hautabadilisha ukweli kuhusu Jerusalem kwasababu ni mji wa wakristo na waislamu na mji mkuu wa taifa la baadaye la Palestina. Aidha mapema hapo jana Jumatano baadhi ya wapalestina waliandamana ikiwa ni pamoja na kuchoma moto bendera za Marekani na Israel kupinga hatua ya Marekani kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.
Naye rais wa Ufaransa Emanuel Macron amesema uamuzi wa Trump unakwenda kinyume na sheria ya kimataifa na azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Macron amesema hadhi ya Jerusalem inapaswa kuamuliwa na waisrael na wapalestina katika mazungumzo yatakayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu katika taarifa yake amesema tangazo hilo la Trump ni hatua muhimu katika mchakato wa amani.
Ama kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Uturuki ameshutumu uamuzi huo wa rais Donald Trump na kusema ni uamuzi ambao haukupaswa kutolewa.
Urusi mwanzoni mwa mwaka huu ilitangaza kuwa inalitambua eneo la magharibi mwa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel na siyo eneo la mashariki ambalo linakaliwa na Israel.
Wakati huohuo baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linatarajia kukutana katika kikao cha dharula ikiwa ni baada ya Trump kutoa tangazo la kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.
Mwandishi: Isaac Gamba/ dw/dpae/ape/rtre