1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Uzinduzi wa awamu ya pili ya chanjo ya Covid-19

Veronica Natalis23 Desemba 2021

Serikali ya Tanzania imezindua awamu ya pili ya chanjo dhidi ya Corona. Huku kukiwa na ongezeko la maambukizi nchini humo, baada ya wabunge wa Kenya na Uganda kudai kuambukizwa.

https://p.dw.com/p/44mDi
Tansania Daressalam | Coronavirus | Impfung Samia Suluhu Hassan, Präsidentin
Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Japo hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na sekretarieti ya jumuiya ya Afrika Mashariki yenye makao yake makuu mjini Arusha, lakini mamlaka katika nchi za Kenya na Uganda zimethibitisha kupitia vyombo vya habari kwamba wabunge wao wamekutwa na maambukizi ya Corona baada ya kutoka hapa mjini Arusha walikokuwa wakihudhuria michezo ya bunge hilo.

Msemaji wa bunge la Uganda, Chris Obore, aliviambia vyombo vya habari nchini humo kwamba wabunge wa Uganda 38 pamoja na wafanyakazi wengine wa bunge walikutwa na maambukizi hayo huku hali zao zikiendelea vizuri.

Kampeni ya chanjo dhidi ya Corona

Tansanina | COVID-19 Impfstoff aus der COVAX Initiative
Picha: Domasa Sylivester/AP/picture alliance

Wakati wa uzinduzi cha chanjo ya Corona awamu ya pili iliyofanyika kitaifa hapa mjini Arusha, Waziri wa Afya, Dk. Doroth Gwajima, alisema maambukizi ya Corona yanaongezeka kwa kasi kutokana na baadhi ya watu kutochukua tahadhari za kujikinga, ambapo mpaka kufikia Disemba 18, 2021, watu 28,214 walishaambukizwa na zaidi ya 700 kupoteza maisha.

Michezo hiyo iliyofanyika tarehe 9 Disemba na kuwahusisha wabunge wa nchi sita wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iliratibiwa na ofisi ya bunge la jumuiya hiyo, japo juhudi za kumtafuta msemaji wa bunge ili kutolewa ufafanuzi suala hilo hazikufanikiwa. Mbunge wa bunge la Afrika Mashariki Pamela Maasai kutoka Tanzania alikuwa ni miongoni mwa wabunge walioshiriki michezo hiyo.

Hivi karibuni wizara ya afya  kupitia ofisi ya mpango wa taifa wa chanjo ilisema kulingana na takwimu za wizara hiyo asilimia 80 ya Watanzania walioambukizwa virusi vya Corona hawakufika hospitali tangu janga hilo lilipogundulika mwishoni mwa mwaka 2019.