1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Taliban kubadili mfumo wa usalama ulioachwa na Marekani?

26 Septemba 2023

Utawala wa Taliban umesema unaunda mtandao mkubwa wa ufuatiliaji wa kamera katika miji ya Afghanistan, ambao unaweza kubadilisha mfumo wa usalama ulioanzishwa na Marekani kabla ya kujiondoa nchini humo mnamo mwaka 2021.

https://p.dw.com/p/4Wp7s
Mpiganaji wa Taliban akiwa katika doria moja ya kitongoji katika jiji la Kabul
Mpiganaji wa Taliban akiwa katika doria moja ya kitongoji katika jiji la KabulPicha: Ebrahim Noroozi/AP/picture alliance

Hata hivyo watetezi wa haki na wakosoaji wa serikali wanahofia kwamba ufuatiliaji huo unaweza kulenga asasi za kiraia na waandamanaji. 

Utawala wa Taliban umekuwa ukisema hadharani kwamba unalenga kurejesha usalama katika taifa hilo na kwamba wameshauriana na kampuni ya kutengeneza vifaa vya mawasiliano ya China ya Huawei kuhusu uwezakano wa ushirikiano.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ushirikiano kati ya Taliban na mataifa mengi ya kigeni kama vile China na Marekani unahusisha kuzuia mashambulizi kutoka kwa makundi ya wapiganaji wa kimataifa kama vile kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS.

Soma pia:Taliban yakanusha madai ya Pakistan kuwa kundi hilo linafanya mashambulizi kwenye mipaka

Lakini baadhi ya wachambuzi wanahoji jinsi gani serikali ya Taliban ambayo inakabiliwa na changamoto za kifedha itaweza kufadhili programu hizo huku makundi ya haki yakielezea wasiwasi kwamba rasilimali zote zitatumika katika kukandamiza waandamanaji.

Hata hivyo maelezo kuhusu jinsi kundi la Taliban linanuia kupanua na kudhibiti kiasi kikubwa cha ufuatiliaji, ikiwa ni pamoja na kuhusisha mpango wa Marekani, bado hayajawekwa wazi.

Taliban: Huu ni mkakati mpya wa usalama

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani wa Afghanistan Abdul Mateen Qani amesema kwambampango wa usambazaji wa kamera kwa wingi ambao utazingatia "maeneo muhimu" mjini Kabul na kwingineko, ni sehemu ya mpya ya mkakati wa usalama ambao utachukua miaka minne kukamilika.

Mpiganaji wa Taliban akilinda usalama jiji la Kabul
Mpiganaji wa Taliban akilinda usalama jiji la KabulPicha: Ebrahim Noroozi/AP/dpa/picture alliance

Aidha msemaji huyo amedokeza kwamba kwa sasa wataalamu wa usalama wanashughulikia ramani ya usalama katika mji wa Kabul na kufikia sasa tayari wana ramani mbili ambazo moja ilitengenezwa na Marekani kwa serikali iliyopita na ya pili kutoka kwa Uturuki.

Lakini hakutoa maelezo zaidi lini Uturuki ilitengeneza ramani hiyo.

Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema nchi hiyo haina "ushirikiano" na Talibanna imeweka wazi kwa kundi hilo kwamba ni wajibu wao kuhakikisha kwamba hawahifadhi magaidi.

Soma pia:WFP kupunguza misaada ya chakula kwa mamilioni ya watu wa Afghanistan

Qani alisema Taliban walifanya "mazungumzo mepesi " kuhusu uwezekano wa ushirikiano na kampuni ya Huawei mnamo Agosti, lakini hakuna mikataba au mipango madhubuti iliyofikiwa.

Mnamo Agosti shirika la habari la Bloomberg liliripoti kwamba Huawei ilikuwa imefikia "makubaliano ya maneno" na Taliban kuhusu mkataba wa kuweka mfumo wa ufuatiliaji.

Lakini msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema hakuwa na ufahamu wa majadiliano maalumlakini aliongeza kusema kwamba daima China imekuwa ikiunga mkono mchakato wa amani na mwanzo mpya nchini Afghanistan na inaunga mkono kampuni za China kutekeleza ushirikiano wa vitendo unaofaa.

Wingi wa kamera Kabul watishia Taliban?

Kulingana na Taliban kuna zaidi ya kamera 62,000, mjini Kabul na miji mingine ambazo zinafuatiliwa kwa pamoja kutoka kwa chumba kikuu cha ufuatiliaji na kulingana na serikali ya zamani ya Afghanistan sahihisho kuu la mwisho la mfumo wa kamera wa Kabul lilifanywa mwaka 2008.

Askari jeshi akiwa katika majukumu yake mjini Kabul
Askari jeshi akiwa katika majukumu yake mjini KabulPicha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Kwa upande mwengine watetezi wa haki na wakosoaji wa serikali wanahofia kwamba ufuatiliaji ulioimarishwa unaweza kulenga asasi za kiraia na waandamanaji. 

Ingawa kundi la Taliban mara kadhaa hukiri kukamata watu, Kamati inayolinda wanahabari imesema angalau waandishi wa habari 64 wamewekwa kuzuizini tangu taliban ilipochukuwa udhibiti.

Soma pia:Taliban yasaini makubaliano yenye thamani ya dola bilioni 6.5 nchini Afghanistan

Taliban inakanusha vikali kuwa mfumo wa ufuatiliaji ulioboreshwa utakiuka haki za Waafghanistan.

Qani alitetea mfumo huo akisema utaendeshwa kama ilivyo katika miji mengine mikubwa na utaendeshwa kwa kufuata Sharia ya Kiislamu, ambayo inazuia kurekodi katika maeneo ya kibinafsi.

Wachambuzi wa masuala ya usalama hata hivyo wanahoji kwamba mpango huo unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kukatika kwa umeme mara kwa mara kila siku nchini Afghanistan, hii ikimaanisha kwamba kutakuwa na changamoto ya ufuatiliaji thabiti. 
 

Wanawake wa Afghanistan waelezea maisha yao kupitia uchoraji