1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yakataa waangalizi wa UN kwenye maeneo salama

Zainab Aziz
8 Mei 2017

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid Muallem amesema nchi yake imekatalia mbali wasimamizi wa Umoja wa mataifa au vikosi vya kimataifa kusimamia maeneo manne ya yaliyotengwa kwa usalama wa raia

https://p.dw.com/p/2ccup
Syrien Jugendliche Parkourläufer
Picha: Reuters/A. Al-Faqir

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Syria amesema Syria haitakubali mabadiliko yoyote mbali na yale yaliyokubaliwa na kutiwa saini na Urusi, Iran na Uturuki katika mji wa Astana nchini Kazakhstan.  Makubaliano hayo yalikuwa ni juu ya kutenga maeneo manne ya usalama ambapo pande zote zitasitisha mashambulio katika maeneo hayo pi sehemu hizo zitagawanywa kwa kuwekwa mipaka ya kiusalama yenye sehemu za kukagua watu kabla hawajavuka maeneo hayo ambapo wanajeshi wadhamini watasimamia kutokana na makubaliano hayo.

Makubaliano hayo yalianza kufanya kazi mnamo siku ya Jumamosi na yameleta hali ya utulivu.  Waziri wa mambo ya nje wa Syria amesema majeshi ya nchi yake yatajibu mashambulio yoyote au pindi makubaliano hayo yatakapovunjwa. Moallem amesema makubaliano hayo yatawezesha kusitishwa mapigano kufikishwa kwa haraka misaada ya kiutu na kuwapa wakimbizi wa ndani nafasi ya kuyafikia maeneo salama ambayo yametengwa katika mikoa minane ya nchini Syria.

Ijapokuwa serikali ya Syria na makundi ya waasi hawakutia saini moja moja makubaliano hayo yaliyofikiwa katika mji wa Astana, waziri wa mambio ya nje wa Syria Walid Muallem amesema leo serikali ya Syria imepitisha maamuzi hayo.

Syrien Damaskus Außenminister Walid al-Mualim
Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid al-MualimPicha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Al Muallem amesema serikali yake imetafuta njia mbadala baada ya mazungumzo ya kutafuta amani kushindikana kwa hivyo serikali yake imekuwa inatekeleza makubaliano na maridhiano ya ndani ya nchi. 

Makubaliano hayo hayazingatii maeneo ambako kwa sasa vita dhidi ya wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS vinaendelea katikati ya Syria na katika maeneo ya Mashariki na Kaskazini.  Wapiganaji wa IS wanakabiliwa na mashambulio makali kutoka kwa vikosi vya serikali ya Syria, wapiganaji wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani na vilevile kutoka kwa wapiganaji wa Kiarabu wanaojulikana kama Syrian Democratic Forces SDF.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Syria Walid Muallem amesema mapambano yanayoendelezwa na kikosi cha SDF dhidi ya kundi la IS ni sawa kabisa na serikali yake inatambua na kuunga mkono vita hiyo. Pili Muallem amesema iwapo raia wa Kikurdi walio nchini Syria wanashiriki katika mapambano dhidi ya IS vilevile ni hatua ambayo inakubalika kisheria kwa sababu Wakurdi hao wanapambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu la IS ndani ya ardhi ya Syria. Watu zaidi ya 320,000 wameuwawa nchini Syria tangu mgogoro kuzuka nchini humo mnamo mwaka 2011.

Mwandishi:Zainab Aziz/APE/AFPE

Mhariri:Josephat Charo