1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Steinmeier na Solana ziarani Moscow

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, na kiongozi wa Umoja wa Ulaya anayehusika na sera ya kigeni, Javier Solana, wamo mjini Moscow hii leo kwa mazungumzo kuhusu jimbo la Kosovo na mzozo wa mashariki ya kati.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamo mjini Moscow kujaribu kupunguza tofauti zilizopo kati ya umoja huo na Urusi kuhusu hali ya baadaye ya jimbo la Kosovo. Ujumbe huo unaojulikana kwa jina, Troika, unawajumuisha waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, kiongozi wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana na kamishna wa umoja huo anayehusika na mahusiano na mataifa ya kigeni, Benita Ferrero Waldner.

Viongozi hao watafanya mazungumzo na waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, katika ziara yao ya siku moja mjini Moscow. Waziri Steinmeier ni miongoni mwa ujumbe huo wa Umoja wa Ulaya kwa sababu Ujerumani ni rais wa umoja huo.

Siku tatu zilizopita mjumbe wa Umoja wa Mataifa aliwasilisha pendekezo la kuifanya Kosovo iwe huru kutoka kwa Serbia. Urusi, mshirika wa jadi wa Serbia, inapinga mpango huo na huenda itumie kura yake ya turufu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kulitilia guu pendekezo la uhuru wa Kosovo. Alipoulizwa kuhusu ushirikiano wa Urusi na Umoja wa Ulaya kuhusu swala la Kosovo, afisa wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya amesema mazungumzo ya leo mjini Moscow yatatoa mwelekeo kuhusu ushirikiano baina ya pande hizo mbili.

Katika mahojiano yake yaliyochapishwa leo na gazeti la Vremya Novostei nchini Urusi, Solana amesema Kosovo ni swala tete linaloikabili Ulaya mwaka huu. Aidha Solana amesema Urusi ni mwanachama wa kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, na inabeba jukumu maalumu kuhusu hali ya baadaye ya Kosovo.

Mkutano wa leo mjini Moscow utazungumzia pia maswala ya nishati. Wasiwasi wa Umoja wa Ulaya umezidi kuhusu kuendelea kuitegemea Urusi kama mtoaji mkubwa wa nishati, kufuatia mizozo ya bei baina ya Urusi na mataifa yanayopitisha nishati, iliyosababisha kutatizwa kwa ugavi wa mafuta na gesi asilia katika nchi za Ulaya Magharibi. Umoja wa Ulaya unataka Urusi ihakikishe itaendelea kutegemewa kama msambazaji mkubwa wa nishati.

Marufuku ya nyama kutoka Poland isiuzwe nchini Urusi ni mada nyengine itakayojadiliwa katika mkutano wa leo mjini Moscow. Marufuku hiyo imekwamisha mazungumzo ya ushirikiano baina ya Urusi na Umoja wa Ulaya. Maofisa wa Umoja wa Ulaya wanasema mzozo kuhusu nyama ya Poland unaelekea kupata ufumbuzi ila kwa mwendo wa kinyonga. Urusi inasema ina wasiwasi kuhusu usalama wa nyama inayotoka Poland lakini wanasiasa wengi nchini Poland wanaamini Urusi inatumia marufuku hiyo kama silaha ya kisiasa.

Serikali ya mjini Warsaw inatumia kura yake ya turufu kuzuia kuanza kwa mazungumzo kuhusu ushirika baina ya Umoja wa Ulaya na Urusi mpaka Moscow ifutilie mbali marufuku hiyo. Wachunguzi wa Urusi wanatarajiwa kwenda Poland wiki hii kutathimini usafi wa vyakula nchini humo.

Ujumbe wa Ulaya unafiri kwenda Ukraine hapo kesho kabla kwenda nchini Serbia kesho kutwa.

 • Tarehe 05.02.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHKm
 • Tarehe 05.02.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHKm

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com