1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kuadhimisha jitihada za kiutu yaadhimishwa leo, Goma

19 Agosti 2010

Kauli mbiu mwaka huu ni 'mimi ni msamaria mwema'

https://p.dw.com/p/OrJH
Maadhimisho hayo yanafanyika mjini Goma, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.Picha: AP

Umoja wa mataifa kwa ushirikiano na mashirika mengine ya kutoa misaada, leo unaadhimisha siku ya jitihada za kiutu duniani huku visa vya kuwawa kwa wafanyakazi wa mashirika ya misaada vikiongezeka. Maadhimisho hayo yanafanyika katika mji wa Goma, Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ikiwa ni saa chache tu baada ya waasi mjini humo kuwauwa wanajeshi watatu wa kulinda amani wa Umoja huo.

Tarehe hii ya maadhimisho ya shughuli za misaada ya kiutu ilipitishwa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa wa mwaka wa 2008 pia inatoa nafasi ya kumbukumbu ya mwaka wa saba tangu lori lililokuwa na bomu liliporipuka katika hoteli ya Canal mjini Baghdad, Iraq na kuwauwa wafanyakazi 22 wa Umoja huo mwaka wa 2003. Kati ya waliouawa alikuwemo kamishna wa wakati huo wa masuala ya haki za binaadamu, Sergio Vieira de Mello.

Kongo Indien UN Soldaten
Wanajeshi watatu kutoka India wa Umoja huo waliuliwa na waasi wa Mai-mai wiki hii.Picha: AP

Siku hii maalum inadhamiria kuuhamasisha umma kuhusu juhudi za kiutu na kuwakumbuka wafanyakazi waliouawa au kujeruhiwa wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Ujumbe wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha siku hii ni kwamba wafanyakazi wanaotoa misaada ya kiutu wanawakilisha yale yote yaliobora kwa hali ya ubinaadamu. Maadhimisho hayo yanahudhuriwa na afisa wa pili wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, Fidele Sarassoro na waziri wa wizara ya kiutu wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, Ferdinand Kambere.

Ni jana tu ambapo waasi wajulikanao kama Mai-mai, walipoivamia kambi ya wanajeshi wa kulinda amani kaskazini mwa jimbo la Kivu na wakawauwa wanajeshi watatu wa kulinda amani wa Umoja huo.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, mwaka wa 2009 wafanyakazi 109 wa kutoa misaada ya kiutu waliuawa kote ulimwenguni.

Umoja huo pia umeelezea kukerwa kwake na kutekwa nyara kwa wanajeshi wake wawili wa kulinda amani kutoka Jordan wanaoshiriki katika kikosi cha UNAMID kilichopelekwa katika jimbo la Darfur mwaka wa 2008. Maafisa hao wawili, Ahmed Quesi na Nabil Kilani hata hivyo waliachiliwa huru.

Wafanyakazi wa shughuli za utoaji misaada ya kiutu wamekuwa wakiwindwa na kutekwa nyara kuanzia enzi za vita vya Biafra nchini Nigeria kati ya mwaka 1967 hadi 1970, Ethiopia miaka ya themanini na nchini Afghanistan miaka ya tisini.

Kuanzia mwaka wa 1997 hadi 2006 visa vya kuvamiwa kwa wafanyakazi wa kiutu viliongezeka kwa asilimia 77. Mwaka jana wafanyakazi 278 wa kutoa misaada ya kiutu walikuwa waathiriwa wa visa 139 vibaya vya ukosefu wa usalama ikilinganishwa na mwaka wa 1999 wakati wafanyakazi 65 waliathirika na visa 34 vya aina hiyo.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni kuwa ‘mimi ni msamaria mwema'.

Mwandishi, Peter Moss /IPS/AFP/DPA

Mhariri, Abdul-Rahman Mohamed