Sera za Marekani kuelekea Misri | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.08.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sera za Marekani kuelekea Misri

Jitahada za kushughulikia mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati zisigubike dosari za kidemokrasia nchini Misri, kama inavyotokea wakati wa ziara ya hivi sasa ya Rais Hosni Mubarak mjini Washington.

Mada iliyopewa kipaumbele katika mkutano wa marais wa Marekani na Misri,Barack Obama na Hosni Mubarak siku ya Jumanne ni kufufuliwa kwa mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati,kwani katika suala hilo Misri inachukuliwa kama mshirika muhimu wa Marekani. Lakini ushirikiano huo una kasoro yake na unazusha mashaka ya kimsingi kuhusu sera za magharibi katika Mashariki ya Kati.

Watalii wanaokwenda kujionea maajabu ya piramidi mjini Cairo au kustarehe katika pwani ya Bahari ya Shamu, hawahisi kuwa nchi hiyo rasmi, imo katika hali ya hatari tangu miaka 28. Kwani kawaida, mtu huambatanisha hali ya hatari na kuwepo kwa wanamgambo wenye silaha na vifaru vya majeshi barabarani-lakini kwa bahati nzuri hayo si mambo yaliyopo Misri licha ya nchi hiyo kukumbwa na machafuko ya kimkoa na mashambulio kadhaa ya kigaidi.Lakini hali ya hatari kwa wahanga wake, si kitu cha kuonekana machoni, bali ni sababu ya raia kuzidi kufikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi na kuzuiliwa bila kufunguliwa kesi. Misri si nchi tu inayokikuka haki za binadamu na inayofanya uchaguzi wenye mashaka.

Nchi hiyo, chini ya uongozi wa Mubarak vile vile, ina umuhimu wa kimkakati na katika masuala mengi ni mshirika wa maghribi anaeweza kutegemewa.Hiyo ni nchi ya kwanza ya Kiarabu kuwa na mkataba wa amani na Israel tangu mwaka 1979. Na hata hivi sasa ina jukumu muhimu kama mpatanishi kati ya pande zenye mivutano na pia kati ya makundi makuu ya Kipalestina yanayohasimiana.Isitoshe,serikali ya Mubarak kwa vitimbi na ukandamizaji inakizuia chama cha Ndugu wa Kiislamu kushika madaraka nchini Misri. Kama kungefanyika uchaguzi ulio huru kweli,basi chama hicho kinachotazamwa pia kwa wasiwasi na nchi za magharibi, labda kingeweza kujinyakulia ushindi.

Yote hayo yana umuhimu mkubwa kwa Marekani hadi kuifanya Misri mpokeaji mkubwa wa pili wa misaada ya fedha katika kanda hiyo.Lakini, kwa kufanya hivyo, Marekani inasaidia mfumo ambao si mfano mzuri wa demokrasia. Na hivyo, huchochea fikra za hatari kuwa nchi za magharibi katika kanda hiyo zinafuata siasa iliyo na misimamo miwili mbali mbali kuhusu demokrasia. Hakuna njia safi ya kujitoa katika hali hiyo ngumu. Kinachohitajiwa ni mkakati uliozingatiwa vyema kumaliza utawala wa miaka mingi wa Mubarak kupitia mageuzi ya kidemokrasia na kuimarisha jamii za kiraia. Vile vile mshirika ashinikizwe kufanyakazi pamoja na makundi mengine nchini na kuongoza utaratibu ambao hatimae, utamfanya mshirika huyo kuondoka pamoja na kundi lake. Hiyo si kazi rahisi lakini, mchakato wa kuleta mageuzi wenye malengo na matumaini unahitajiwa haraka. Hata kiuchumi, Misri daima ikiwa katika hali ya hatari, haina nafasi nzuri ya kujiendeleza.

Mwandishi: R.Sollich

Mhariri: M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 19.08.2009
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/JE1H
 • Tarehe 19.08.2009
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/JE1H

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com