1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz ayatembelea maeneo ya mafuriko Saxony-Anhalt

Josephat Charo
5 Januari 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ameyatembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko katika jimbo la Saxony-Anhalt kujionea madhila yanayowakabili wakaazi.

https://p.dw.com/p/4ars8
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Jan Woitas/dpa/picture alliance

Scholz aliwahi kuyatembelea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko ya jimbo la Lower Saxony siku moja kabla sikukuu ya mwaka mpya. Kansela huyo ataandandana na Waziri wa Mazingira, Steffi Lemke na Waziri Mkuu wa jimbo la Saxony-Anhalt, Reiner Haseloff.

Wanasiasa hao wanataka kutafuta taarifa zaidi kuhusu hali ya mafuriko huko Oberröblingen ambayo ni wilaya ya Sangerhausen. Scholz alitarajiwa kukutana na mkuu wa wilaya ya Mansfeld-Südharz, André Schröder kwenye daraja la Helme ambalo linakabiliwa na hatari ya kuanguka.

Mazungumzo yalitarajiwa pamoja na kamanda anayefuatilia janga la mafuriko, mashirika ya kutoa huduma za dharura na mameya wa miji iliyoathiriwa. Scholz, Lemke na Haseloff wanatarajiwa pia kukitembelea kituo cha kujaza mchanga kwenye magunia katika kijiji cha Berga na kuzungumza na wafanyakazi wa kujitolea.