1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarkozy na Brown wasema watakua tayari kwenda Darfur

Mohammed Abdu-Rahman20 Julai 2007

Ufaransa na Uingereza kudhamini mswada wa azimio la umoja wa mataifa juu ya jamani katika imbo hilo la magharibi mwa Sudan.

https://p.dw.com/p/CHAl

Rais wa Ufaransa Nikolas Sarkozy na Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown wamekua na mazungumzo mji ni Paris leo kuzungumzia maswala kadhaa. Aidha walitangaza pia kwamba wako tayari kufanya ziara ya pamoja kulizuru eneo la magharibi wa Sudan la Darfur, kuupa msukumo utaratibu wa kusaka amani katika jimbo hilo.

Viongozi hao wawili Sarkozy na Brown walisema baada ya mazungumzo yao mjini Paris kwamba, Ufaransa na Uingereza zitaungana kudhamini azimio la umoja wa mataifa kutaka kutumwa jeshi la pamoja la umoja wa Afrika na umoja wa mataifa huko Darfur. Rais Sarkozy akatamka kwamba “ ikiwa azimio hilo litapitishwa, tuko hata tayari kwenda Darfur, Chad na Sudan.”

Akaongeza kwamba wanaamini kwa kushirikiana wanaweza kufanikisha kupatikana azimio la umoja wa mataifa , litakalotoa nafasi ya kutumawa jeshi hilo la pamoja kati ya umoja wa afrika na umoja wa mataifa katika jimbo hilo la magharibi mwa Sudan , huku Waziri mkuu Brown akisema wanataraji azimio hilo litapitishwa haraka.

Baraza la usalama la umoja wa mataifa linazingatia mswada awa azimio wa kurasa tano uliodhaminiwa na Uingereza, Ufaransa na Ghana ambao Sudan na wanachama wengine wa baraza hilo wanasema unahusiana na maelezo mengi juu ya masuala ya kiutu na mengineyo, kikiwemo kitisho cha hatua zaidi pindi upande wowote miongoni mwa zinazohusika utashindwa kutoa ushirikiano na kuwajibika. Azimio hilo litaithinisha kutumwa wanajeshi na polisi jumla ya 26,000 kutoka umoja wa afrika na umoja wa mataifa na mpango huo kugharimu zaidi ya dola bilioni mbili katika mwaka wa kwanza.

Bw Brown alisema kupatikana kwa azimio hilo, kutatuma ujumbe kwamba hatimae utaratibu wa amani unasonga mbele na kwamba watashiriki katika ujenzi wa uchumi wa eneo hilo. Akasema kwamba yeye pamoja na Rais Sarkozy watayafuatilia matukio kwa makini kuhakikisha Sudan inachukua hatua zinazohitajika kuondoa maafa yanayoukumba umma wa Darfur.

Juhudi za kibalozi kuhusu mzozo wa Darfur zimekua zikiendelea na wiki iliopita mkutano wa kimataifa uliotishwa Libya, chini ya uwenyekiti wa wajumbe wanaohusika na mzozo huo wa umoja wa afrika na umoja wa mataifa Dr Salim Ahmed Salim na Jan Eliasson,ulipata mafanikio baada ya waasi wa chama cha haki na usawa, ambao hawakusaini makubaliano ya amani ya Abuja mei mwaka jana, kukubali kuhudhuria mazungumzo yote yajayo. Waasi hao walikubali kukutana mjini Arusha – Tanzania tarehe 5 mwezi ujao.

Aidha mbali na swala la Darfur,viongozi hao wa Ufaransa na Uingereza walizungumzia mipango ya ushirikiano katika ujenzi wa manowari za kubeba ndege, lakini pamoja na kusisitiza juu ya ushirikiano huo, hawakuweka muda maalum wa kukamilisha mazungumzo ya kiufundi yaliocheleweshwa kwa muda mrefu sasa.

Mipango hiyo inahusiana na ujenzi wa jumla ya manowari tatu, mbili kwa ajili ya Uingereza na moja ya Ufaransa. Wakati wa utawala wa mtangulizi wa Rais Sarkozy, Jacques Chirac na yule wa Brown. Tony Blair, Ufaransa na Uingereza zilikubaliana, kusimamia gharama za mipango hiyo licha ya hali ya kukaza mkwiji panapohusika na matumizi yao ya ulinzi.

Lakini hata hivyo makubaliano ya mwisho yatategemea makubaliano ya kiufundi, kurahisisha sehemu kubwa ya kazi hiyo kwa kiasi kinachowezekana, pamoj a na matatizo ya kaumua nani atakua na jukumu la kutegeneza nini .