1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samia, Museveni na Ruto wakutana kujadili EAC

15 Machi 2024

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekutana na wenzake wa Uganda, Yoweri Museveni na William Ruto wa Kenya, kujadiliana juu ya mustukabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

https://p.dw.com/p/4ddhN
Signing ceremony of the treaty of accession by the Federal Republic of Somalia into EAC
Picha: Presidential Press Unit Uganda

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ilisema, viongozi hao pamoja na kujadiliana kuhusu mtengamano wa Jumuiya hiyo, pia walisisitiza umuhimu wa kuharakishwa hatua ya ukusanyaji maoni ya wananchi ili kufikia hatma ya kuundwa shirikisho la kisiasa la Jumuiya hiyo.

Taarifa inasema, viongozi hao watatu ambao mkutano wao haukutangazwa; wanataka maoni ya wananchi yaakisi namna wanavyotaka juu ya muundo pamoja na maeneo yanayopaswa kuangaliwa wakati wa kuandaa rasimu ya shirikisho hilo la kisiasa.

Imefahamika kuwa hatua kama hiyo tayari imefanyika katika nchi za Burundi, Kenya na Uganda lakini  bado haijafahamika hatma ya nchi nyingine wanachama ikiwamo Rwanda na Sudan Kusini zilizosajiliwa ndani ya jumuiya hiyo zaidi ya miaka mitano iliyopita.

EAC yakanusha kudumaa kiuchumi

Kuanzishwa kwa mchakato huo kunaweza kuibua hisia nyingine nchini Tanzania ambayo raia wake wamekuwa na wasiwasi wa huenda rasimali kubwa ya ardhi yake ikawa mikononi mwa wageni. Hali hiyo inatajwa kukwamisha mchakato wa awali ulioanzishwa wakati wa utawala wa awamu ya nne.

Akilitazama suala hilo, mhadhiri wa chuo cha diplomasia, Dinnis Konga anasema ingawa wananchi wako tayari kuingia katika shirikisho, kigugumizi kuhusu jambo hilo bado kinaendelea kusalia miongoni mwa wananchi wengi.

Mchakato unafanyika wakati mivutano ikiendelea kushuhudiwa

Tanzania | Jumuiya ya EAC
Baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EACPicha: Philbert Rweyemamu/EAC

Ama Msukumo unaotolewa na viongozi hao kuhusu kuharakishwa mchakato wa shirikisho la kisiasa unakuja katika wakati ambapo mivutano kati ya baadhi ya nchi wanachama ikiendelea kutokota.

Kumekuwa na ukosoaji unaotolewa na baadhi ya wachambuzi wa mambo wakilaumu kukosekana kwa utashi wa kisiasa ndani ya viongozi wa nchi wanachama kuitafutia majawabu ya mizozo hiyo kabla haijavuka mipaka. Mataifa kama DR Kongo, Burundi na Rwanda yamekuwa katika mivutano ya muda mrefu na Jumuiya yenyewe haijatoka hadharani kulizungumzia suala hilo.

Viongozi wa EAC wakutana Dar es Salaam

Kwa maoni yake mchambuzi wa mambo, Nicolas Clinton anasema hali hiyo inatoa ishara pengine viongozi ndani ya jumuiya hiyo hawatembei katika kauli moja.

Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki iliyoasisiwa na nchi wanachama watatu, Tanzania, Kenya na Uganda hili itakuwa jaribio lake la pili kutaka kufufua shirikisho la kisiasa baada ya kuasisiwa upya mwaka 1996 baada ya ile ya awali kuvunjika.

Mwandishi: George Njogopa