1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RIYADHI: Umoja wa Ulaya wataka wakuu wa kiarabu kupanua wigo wa kutafuta amani mashariki ya kati

28 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCEy

Mkuu wa siasa za nje katika Umoja wa Ulaya, Javier Solana, yuko mjini Riyadhi Saudi Arabia, ambapo amewataka viongozi wa nchi za Kiarabu, kupanua wigo wa kutafuta amani Mashariki ya Kati, na kusema umoja huo unaunga mkono juhudi hizo.

Solana ambaye yuko mjini Riyadhi kuhutubia mkutano wa kila mwaka wa wakuu wa nchi za Kiarabu, amesema kuwa mkutano wa kimataifa wa pande nne zinazosaka amani mashariki ya kati, kwa msaada wa nchi za kiarabu unaweza kupiga hatua katika suala hilo.

Pande hizo nne ni pamoja na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Urusi na Marekani.

Javieir Solana amesema kuwa mkutano ujayo wa pande hizo nne umepangwa kufanyika katikati ya mwezi ujayo huko Misri.

Mapema kabla ya mkutano huo wa siku mbili wa wakuu wa kiarabu unaoanza leo, mawaziri wa nje wa nchi hizo, walikubaliana kufufua mpango wao wa amani ambao unatoa nafasi kwa Israel kuwa na uhusiano kamili na nchi hizo, lakini iwapo tu, nchi hiyo itayaachia maeneo yote iliyoyateka mwaka 1967, na kuruhusu kuanzishwa kwa dola ya Palestina na kurejea kwa wakimbizi wa kipalestina.

Israel iliukataa mpango huo hapo mwanzo, lakini katika siku za hivi karibuni viongozi wake wamesema kuwa mpango huo ni mwanzo wa mazungumzo.