1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Marekani azungumza na Mahmud Abbas

Oummilkheir25 Septemba 2007

Uwezekano upo wa kuundwa taifa la Palastina, jirani na Israel.

https://p.dw.com/p/CH7l
Picha: AP

Rais George W. Bush wa Marekani amezungumzia dhamiri zake za kufanya kila liwezekanalo ili taifa la Palastina liundwe karibu na Israel .Rais Bush aliyesema hayo mwishoni mwa mazungumzo pamoja na rais wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas amesema ”lengo hilo linaweza kufikiwa”.

“Nnaunga mkono kwa nguvu dola la Palastina liundwe” amesema rais Bush aliyeonana na rais wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas na waziri mkuu Salam Fayyad mjini New-York ,ili kushadidia mpango wa Marekani wa kuitisha mkutano wa kimataifa kuhusu amani ya mashariki ya kati.

Rais huyo wa Marekani amesema anaamini,rais Mahmoud Abbas na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert wanahamu ya kuishi pamoja kwa amani mataifa mawili-Palastina na Israel.”Nimemwambia rais Abbas,Marekani itafanya kila liwezekanalo kusaidia kutekeleza azma hiyo.”Amesema kiongozi huyo wa Marekani na kuongeza tunanukuu:”Nnaamini fikra ya kuwepo madola mawili ,jirani na yanayoishi kwa amani inaweza kutekelezwa”-mwisho wa kumnukuu kiongozi huyo wa Marekani aliyekutana baadae na mjumbe maalum wa kimataifa katika eneo la mashariki ya kati,waziri mkuu wa zamani wa Uengereza Tony Blair.

“Tunategemea uungaji mkono wako na tunaamini juhudi zako zitaleta amani ya haki na ya kudumu Mashariki ya kati.”Amesema kwa upande wake rais wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas aliyezungumzia “matumaini mema” kufuatia mwito alioutoa rais Bush,July iliyopita ,wa kutisha mkutano wa kimataifa kuhusu amani ya mashariki ya kati.

Mkutano huo ni sehemu ya juhudi za rais Bush za kuufufua utaratibu uliokwama wa amani kati ya Israel na Palastina.Hata baadhi ya washirika wa Marekani wamekua wakimlaumu kwa kuupa kisogo mzozo huo unaendelea tangu miaka 60 hivi sasa.

Wiki iliyopita rais George W Bush alimtuma waziri wake wa mambo ya nchi za nje wa Marekani,bibi Condoleezza Rice mashariki ya kati ili kuandaa uwanja kuweza kuitishwa mkutano huo.Mwezi ujao,bibi Laura Bush anatazamiwa pia kulitembelea eneo hilo kwa ziara ya kidiplomasia iliyolengwa kutakasa hadhi ya Marekani katika eneo la Mashariki ya kati.

Akizungumza kuhusu mkutano huo wa Mashariki ya kati uliopangwa kuitishwa mwezi November ujao,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice amesema: “Mpango wa amani wa pande nne bado ni muongozo wa kuaminika unaoungwa mkono na jumuia ya kimataifa,juu ya namna ya kuundwa dola la Palastina.”

Wakati huo huo muasisi mmojawapo wa chama cha ukombozi wa Palastina ,Dr.Haidar Abdel Chafi amefariki dunia alfajiri ya leo akiwa na umri wa miaka 84.

Mwanasiasa huyo alijipatia sifa ulimwenguni alipoongoza ujumbe wa Palastina katika mazungumzo ya amani ya Madrid mwaka 1991 pamoja na Israel.Aliwahi pia kuteuliwa na Yasser Arafat kuongoza ujumbe wa Palastina katika mazungumzo ya amani yaliyodumu miaka miwili mjini Washington.