1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Sarkozy ziarani Senegal na Gabon

Saumu Mwasimba26 Julai 2007

Ziara hiyo inafanyika baada ya hapo jana kuwa nchini Libya na kutiliana mikataba kadhaa na rais Muammar Gaddafi wa nchi hiyo

https://p.dw.com/p/CB2R
Rais Nicolas Sarkozy na kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi
Rais Nicolas Sarkozy na kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: AP

Rais wa ufaransa Nicolas Sarkozy ameondoka Tripoli baada ya mazungumzo yake na kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi na kulekea Senegal kwa ziara ya kwanza barani Afrika kusini mwa jangwa la sahara tangu achaguliwe kuwa rais wa Ufaransa mwezi mei.

Rais Sarkozy aliwasili Tripoli hapo jana ikiwa ni siku moja baada ya ufaransa ikishirikiana na Umoja wa ulaya kufanikisha kuachiwa Huru wahudumu sita wa sekta ya afya wakibulgaria waliohukumiwa kifungo cha maisha kwa kuwaambukiza kwa makusudi virusi vya HIV watoto 400 kutokana na damu iliyokuwa inavirusi hivyo.

Adhabu hiyo ilitolewa baada ya ile ya kifo kubatilishwa.

Katika mazungumzo yake na viongozi wa Libya hatimaye nchi hizo mbili zilitiliana saini mikataba ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na katika sekta ya afya,elimu kudhibiti wahamiaji , vita dhidi ya ugaidi na ulinzi.

Aidha pande hizo mbili zimezungumzia pia masuala ya nishati ya Nuklia kwa matumizi ya amani.

Akizungumzia juu ya utiaji saini wa mikataba hiyo rais Sarkozy alisema ’Bila shaka na Ufaransa inataka kuwa na ushirikiano na Libya lakini sio sisi pekee yetu. Marekani imeshafanya hivyo, Tony Blair alishakuweko Libya na hata bwana Prodi pia sasa kwanini Ufaransa ibakie Kando?’’

Itakumbukwa kwamba Libya iliachana na mpango wake wa Nuklia na utengenezaji wa silaha za maangamizi mwaka 2003 hatua iliyofungua milango ya kuanza kuimarika taratibu kwa uhusiano kati ya nchi hiyo na nchi za Magharibi.

Rais Sarkozy aliwahi kuitembela libya mwaka jana wakati akiwa waziri wa mambo ya ndani. kiongozi huyo wa Ufaransa sasa ameelekea Senegal na baadae ataizuru Gabon zote mbili makoloni ya zamani ya Ufaransa barani humo.

Miongoni mwa yale yanayotazamiwa kujadiliwa akiwa mjini Dakar ni ushirikiano katika kudhibiti wimbi la wahamiaji wanaojaribu kuingia katika nchi za ulaya kwa njia ya bahari.

Wakati huo huo makundi ya wanaharaki wanaotetea haki za binadamu wamemtaka bwana Sarkozy aishinikize Senegal katika mazungumzo yake na rais Abdillahi wade iharakishe kesi inayomkabili kiongozi wa zamani wa Chad Hissane Habre juu ya ukiujaki wa haki za binadamu pamoja na kutoweka kwa idadi kubwa ya wapinzani wakati wa utawala wake.

Habre ambaye amekuwa akiishi uhamishoni nchini Senegal tangu alipoangushwa madarakani yuko gerezeni kufuatia warranti uliowasilishwa na Mahakama moja ya Ubelgiji iliyoitaka Senegal imkabidhi kujibu mashtaka yaliyofunguliwa na baadhi ya wahanga wa utawala wake.

Lakini Senegal pamoja na kutakiwa na tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Afrika kuharakisha kesi dhidi ya Habre imekataa kumkabidhi ikisema anapaswa kuhukumiwa nchini humo lakini pamoja na hayo imedai kwamba utata uliopo katika katiba ya nchi hiyo unalifanya suala hilo kuwa gumu kulitekelza kwa haraka.