1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Saleh apata ahuweni

10 Juni 2011

Wafuasi wa pande zote mbili zinazopingana nchini Yemen, leo hii (10.06.2011) wanafanya maandamano mapya mjini Sanaa, baada ya tangazo kuwa hali ya kiafya ya Rais Ali Abdullah Saleh inaimarika baada ya kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/11Y0Z
Rais Ali Abdullah Saleh
Rais Ali Abdullah SalehPicha: AP

Ijumaa ya leo, kama zilivyo kawaida za Ijumaa nyengine zilizopita, inatarajiwa kushuhudia maandamano makubwa kwa wanamageuzi na wafuasi wa serikali, kila upande ukishikilia msimamo wake.

Ambapo wafuasi wa Rais Saleh wanasherehekea kupona kwa kiongozi wao, wa upinzani wanapinga kurejea kwake nchini kutokea Saudi Arabia anakotibiwa.

Usiku wa kuamkia jana, mpwa wa Rais Saleh, Yahya Saleh, alisema kwamba mjomba wake anaendelea vyema.

"Rais anaendelea kutibiwa na hali yake inaendelea vizuri kutoka majeraha yaliyosababishwa na magaidi. Ndani ya kipindi cha wiki mbili atakuwa amesharudi hapa Sanaa. Nchi yake inamsubiri kwa hamu, na atakuja kuendelea kutawala." Alisema Saleh.

Taarifa kama hizi zilizotangazwa na televisheni ya serikali, Saba'a, zilishangiliwa na wafuasi wake kwa milio ya risasi ambayo, hata hivyo, inaripotiwa kuwajeruhi watu 80 katika mji mkuu wa Sanaa peke yake. Mashahidi wanasema kuwa, kuna maafa mengine pia katika miji mengine ya Yemen.

Hapo jana, vikosi vitiifu kwa Rais Saleh, viliwauwa wapiganaji wawili wa upinzani kwenye mji wa kusini wa Taez. Katika mji mwengine wa Zinjibar, mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji, wanaoshukiwa kuwa ni Al-Qaida, yamekuwa yakiendelea tangu mwezi uliopita.

Mashambulio ya vikosi vya serikali yaliungwa mkono pia na ndege za jeshi la Marekani, ambazo zilirusha makombora kwenye mji huo. Marekani inadai kwamba inafanya mashambulio hayo ili kuwazuia wafuasi wa Al-Qaida kuitumia fursa ya machafuko nchini Yemen kujiimarisha.

Likiwanukuu maafisa wa serikali ya Marekani waliotaka majina yao yasitajwe, Shirika la Habari la AFP limesema kwamba mashambulizi hayo ya Marekani yalianza tangu Ijumaa iliyopita, ambapo kiongozi wa ngazi ya kati wa Al-Qaida, Abu Ali al-Harithi, aliuawa.

Mashambulizi haya ni mlolongo wa mashambulizi ya kushitukizia ya Marekani nchini Yemen, ambapo mwanzoni mwa mwezi uliopita, ndege inayojiendesha yenyewe ilimkosa kiongozi mwengine wa Al-Qaida, Anwar al-Awlaki.

Rais Saleh mwenyewe hajaonekana hadharani tangu mashambulio hayo ya bomu, huku kukiwa na taarifa zinazokinzana tangu apelekwe mjini Riyadh nchini Saudi Arabia kwa matibabu.

Tayari kituo kimoja cha mkakati wa kijeshi na ujasusi cha Marekani, STRATFOR, kimetoa taarifa yake hapo jana kikisema kwamba mashambulio dhidi ya Rais Saleh yalikuwa jaribio la mauaji dhidi yake lililopangwa na kutekelezwa kutoka watu wa ndani ya serikali yake na hayakutokana na roketi lililorushwa kutoka nje ya Ikulu.

STRAFOR inasema taarifa yake inatokana na picha ilizozikusanya katika msikiti uliomo ndani ya makaazi ya Rais Saleh, ambapo mripuko ulitokea mwanzoni mwa mwezi huu. Kwa mujibu wa STRATFOR, matundu katika kuta za msikiti huo yanathibitisha kwamba mripuko ulitokea ndani na sio kwamba ulitokea nje.

Ikiwa kuna lolote ambalo linapatikana kutokana na matokeo haya ya awali ya taasisi hiyo ya mkakati na ujasusi, basi ni ukweli kwamba hata kama Rais Saleh atapona na kurudi Yemen kutawala tena, utawala wake unakabiliwa na mmomonyoko kutokea ndani yake yenyewe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/APE
Mhariri: Othman Miraji