1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais mpya wa Ujerumani apuuza madai

Aboubakary Jumaa Liongo2 Julai 2010

Rais mpya wa Ujerumani Christian Wulff amepuuza madai kuwa ushindi wake mwembamba ni pigo kwa serikali ya mseto ya mrengo wa kati kulia inayoongozwa na kansela Angela Merkel.

https://p.dw.com/p/O8mC
Rais mpya wa Ujerumani Christian WulffPicha: dpa

Mwanasiasa huyo kutoka chama cha  Christian Democrat  alimshinda mgombea wa mrengo wa kati kushoto, Joachim Gauck katika uchaguzi wa urais hapo jana uliyochukua zaidi ya saa tisa na kulazimika kufanyika kwa duru tatu kabla ya mshindi kupatikana.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Ujerumani Bwana Wulff amesema ukweli kuwa mwishowe aliweza kupata wingi wa kura ni kitu kinachompa nguvu na hamasa.

Hata hivyo chama cha Christian Democratic kimekuwa kikitathmini tabia ya baadhi ya wabunge wake kutokuwa na nidhamu na chama. Christian Wulff alifanikiwa kupata ushindi huo dhidi ya Gauck, baada ya Kansela Angela Merkel na viongozi wenzake wa muungano wa vyama vinavyotawala kuomba kuwepo na mshikamano.

Kujiuzulu ghafla kwa Rais Horst Koehler lilikuwa  ni pigo jingine kwa serikali ya Kansela Merkel.

Wakati huo huo kiongozi  ndani ya bunge wa chama cha walinzi wa mazingira , Renate Künast, amesema kushindwa kwa  Joachim Gauck  kumehitimisha mapendekezo yoyote juu ya mustakhbali wa ushirikiano kati ya chama cha upinzani cha SPD chama chake na kile cha mrengo wa shoto, Die Linke.

Mwandishi:Aboubakary Liongo