Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen atibiwa Saudi Arabia
5 Juni 2011Taarifa hizo zimethibitishwa na maafisa wa serikali ya Yemen na Saudi Arabia ambao hawakutaka kufahamika. Duru zinaeleza kuwa baadhi ya maafisa wengine wa ngazi za juu wa serikali ya Yemen nao pia wameeleka Saudi Arabia kutibiwa baada ya eneo la kasri ya Rais Saleh kushambuliwa kwa roketi iliyofyatuliwa na waasi Ijumaa iliyopita wakati wa usiku.
Wahudumu wa usalama wanaripotiwa kuwa waliuawa katika shambulio hilo. Kwa upande mwengine, taarifa za shirika la utangazaji la BBC zinaeleza kuwa Rais Ali Saleh huenda ameteketea vibaya na kupata majeraha karibu na moyo, baada ya shambulio hilo. Katika hotuba yake ya Ijumaa jioni iliyotangazwa na kituo cha redio ya taifa, Rais Saleh alisema hana neno.
Itakumbukwa kuwa wapinzani wa kiongozi huyo wa Yemen, wamekuwa wakiandamana kwa muda mrefu ili kumshinikiza aondoke madarakani hasa baada ya Rais Saleh kukataa katakata kulitia saini pendekezo lililotolewa na Baraza la Mataifa ya Ghuba, GCC. Kulingana na pendekezo hilo, Rais Saleh anapaswa kuachia ngazi pasina adhabu ya mahakama.
Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-ZPR
Mhariri: Kitojo, Sekione