1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olmert na Abbas yaelekea zaidi kwenye njia ya kusaka amani

Maja Dreyer3 Oktoba 2007

Katika mazungumzo yao ya leo, viongozi wa Israel na Palestina, Ehud Olmert na Mahmoud Abbas, waliendeleza mbele zaidi kwenye njia yao ya kufikia makubaliano ya amani. Haya ni kabla ya mkutano wa kilele juu ya amani Mashariki ya Kati utakaodhaminiwa na Marekani mwezi Novemba.

https://p.dw.com/p/CH7B
Lini vita vitaisha?
Lini vita vitaisha?Picha: AP

Mkutano wa leo ulikuwa wa kwanza pamoja na timu maalum za pande zote mbili zilizoundwa kwa azma ya kupatanisha. Ni mkutano wa tano wa ana kwa ana kati ya Rais Mahmoud Abbas wa Palestina na Ehud Olmert, waziri mkuu wa Israel. Baada ya mazungumzo haya yaliyoendelea kwa muda wa saa mbili, David Baker, msemaji wa Ehud Olmert, aliwaambia waandishi wa habari kuwa viongozi hao wawili walikubaliana na matarajio yao ya timu zao ya kufanya mazungumzo mengine magumu katika wiki zijazo kabla ya mkutano mkubwa wa Novemba. Lengo ni kuandaa taarifa ya pamoja.

"§Lengo letu ni kuanzisha mazungumzo yasiyokuwa na mwisho maalum juu ya makubaliano ya kudumu baada ya mkutano wa Novemba," Bw. Baker alisema. Na aliongeza kwamba mazungumzo ya leo yalileta hali ya kuwa na matumaini kabla ya mkutano ujao wa kimataifa.

Waziri mkuu Ehud Olmert anashinikizwa na baraza lake na mawaziri kutoridhia masuala tete na anapendelea makubaliano ya msingi yasiyokuwa na nguvu kabla ya mkutano wa Novemba. Olmert alifunga muungano wa kisiasa pamoja na vyama vyenye misimamo mkali wa kitaifa na kiorthodox ambavyo vinaweza kupinga makubaliano ambayo chama chake na kile cha Labor kingeyakubali.

Rais Abbas wa Palestina, kwa upande wake, anataka makubaliano ya kina yenye ratiba kwa mazungumzo kuhusu masuala ya msingi kama mipaka, mustakabali wa wakimbizi wa Israel na Palestina pamoja na hali ya Jerusalem.

Juhudi za kuuanzisha upya mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel ziliitishwa baada ya Rais Abbas kuliteua baraza la mawaziri linalounga mkonona nchi za Magharibi baada ya Hamas kulidhibiti eneo la ukanda wa Gaza hapo mwezi wa June. Abbas ameeleza kwamba Waisrael na Wapalestina wanaweza kutiliana saini makubaliano ya amani mnamo kipindi cha miezi sita ijayo. Naye waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert pia ameeleza matumaini ya kufikiwa mapatano hayo. Wakati huo huo lakini alijaribu kupunguza umuhimu wa mkutano wa Novemba utakaofanyika Marekani na kusema kwamba zaidi ni mkutano wa kimataifa badala ya mazungumzo ya amani.

Vyombo vya habari vya Israeli leo vilinukuu idara za serikali za Marekani zikisema kwamba mkutano unaotarajiwa kufanyika Novemba huenda utaahirishwa wiki kadhaa ili kuzipa muda zaidi pande hizo mbili. Marekani bado haijatangaza tarehe ya mktutano.

Kama kutoa ishara ya nia njema, Israel imewaachilia huru wafungwa 90 wa Palestina wiki hii, lakini rais Abbas alisema inabidi hatua nyingine ichukuliwe.

Msemaji wa kundi la Hamas linalotawala eneo la ukanda wa Gaza alisema masuala ya msingi kwa Wapalestina hayatazingatiwa kwenye mikutano kati ya Ehud Olmert na Mahmoud Abbas.

Wakati huo huo kwenye ukanda wa Gaza, wanamgambo watatu wa kundi la Hamas waliuawa katika matukio mbali mbali. Mmoja alizikwa alipojaribu kuchimba handaki, mwingine aliuawa katika mapigano na jeshi la Israel na wa tatu aliuawa kwa roketi.