Obama azikosoa sera za Bush nchini Iraq. | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama azikosoa sera za Bush nchini Iraq.

Seneta Barack Obama , mmoja kati ya wagombea watarajiwa katika kinyang’anyiro cha kuelekea kuteuliwa na chama cha Democratic nchini Marekani katika kiti cha urais, amesema siku ya Jumanne kuwa ataifanya Afghanistan lengo la juhudi za Marekani za kupambana na ugaidi pamoja na kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya magaidi katika mpaka nchini Pakistan iwapo serikali ya rais Pervez Musharraf itashindwa kufanya hivyo.

Seneta Obama ( kulia) na seneta Clinton, mawazo yao hayakutani kuhusu kukutana na wale wanaoipinga Marekani.

Seneta Obama ( kulia) na seneta Clinton, mawazo yao hayakutani kuhusu kukutana na wale wanaoipinga Marekani.

Obama ambaye yuko nyuma ya mgombea mwingine Seneta Hillary Clinton katika maoni ya wapiga kura , amezikosoa vikali sera za kupambana na ugaidi za rais George W. Bush, akidai kuwa rais huyo anapigana vita ambayo magaidi wanataka Marekani ipigane.

Bin laden amesema , pamoja na washirika wake wanafahamu kuwa hawawezi kuishinda Marekani katika uwanja wa mapambano ama mapambano kimawazo.

Lakini wanaweza tu kuleta uchokoza ili kuleta hali kama inayotokea nchini Iraq, uvamizi ambao haukupaswa kutokea wa nchi ya Kiislamu ambao umezusha mapigano mapya , na kupunguza uwezo wa jeshi la Marekani, matumizi makubwa ya bajeti, kuleta ongezeko la magaidi, kuitenga Marekani, kuipa demokrasia jina baya, na kusababisha wamarekani kujiuliza kuhusu ushiriki wetu katika masuala mbali mbali duniani.

Kwa kukataa kusitisha mapigano nchini Iraq, rais Bush anatoa kwa magaidi kile ambacho wanakitaka, na kile ambacho baraza la Congress ilipiga kura kuwapatia mwaka 2002, aliongeza katika moja kati ya maelezo yake kadha yanayokumbusha kuwa Clinton alipiga kura kuidhinisha mapambano ya kijeshi, Marekani kuikalia Iraq kwa muda usiojulikana, kwa gharama isiyojulikana, na kwa matokeo ambayo hayajulikani pia.

Obama pia ametoa wito wa kuongezwa kwa misaada pamoja na mikopo kwa nchi masikini hadi kufikia dola bilioni 50 kwa mwaka ifikapo mwaka 2012 ili kupunguza wimbi la hali ya kukata tamaa ambayo inazusha chuki, ikiwa ni pamoja na dola bilioni mbili kwa ajili ya mfuko wa elimu duniani ili kupambana na shule za kidini katika dini ya Kiislamu , madrasa katika mataifa ya Kiislamu.

Hotuba hiyo inakuja katikati ya mvutano baina ya Obama na Clinton , ambao kwa pamoja wanaongoza katika kundi kubwa la wagombea wanane wa chama cha Democratic wanaowania kuteuliwa na chama chao , juu ya ushauri wa kukutana na viongozi wanaoonekana kutofautiana na sera za Marekani kama rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad ama rais wa Venezuela Hugo Chavez bila masharti.

Clinton ameshutumu taarifa za Obama katika mjadala wiki iliyopita kuwa kufanya hivyo itakuwa kutowajibika na kutokuwa na mbinu, shutuma ambazo zimekuwa zikitumiwa na Obama kumlinganisha Clinton na mtazamo wa Bush na makamu wa rais Cheney, mada aliyoitumia sana bila lakini kumtaja Clinton kwa jina katika matamshi yake.

Wagombea wote wamekuwa wakishutumu vikali sera za rais Bush katika vita vya Iraq na walipiga kura wiki iliyopita kuunga mkono sheria ambayo itahitaji rais kuyaondoa majeshi yote ya Marekani ifikapo May 31, wakati akibakisha wanajeshi wachache ili kusaidia kuwafunza Wairaq, kulinda maeneo ya wafanyakazi wa kawaida wa Marekani pamoja na kufanya operesheni dhidi ya wapiganaji wa al-Qaeda, licha ya kuwa Obama siku ya Jumatano alishauri kuwa jeshi litakapowekwa kufanya kazi za kupambana na al-Qaeda linaweza kuwa katika eneo ambalo pengine sio ndani ya Iraq.

Ameongeza kusema kuwa kama rais ataweka mamia ya mamilioni ya dola katika msaada wa kijeshi kwa Pakistan kuwa ya masharti, na ataweka masharti hayo wazi. Pakistan ni lazima ipige hatua muhimu katika kufunga vituo vya mafunzo, kuwaondoa wapiganaji kutoka nje ya nchi hiyo, na kuzuwia Taliban kutumia ardhi ya Pakistan kama sehemu ya kufanyia mashambulizi dhidi ya Afghanistan.

 • Tarehe 02.08.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHA8
 • Tarehe 02.08.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHA8

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com