1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama asema uchaguzi wahusika na mustakabali wa Marekani

27 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CyPP

WASHINGTON:

Nchini Marekani,katika kinyanganyiro cha uteuzi wa mgombea urais,Seneta Barack Obama wa chama cha Democratic ameshinda asilimia 55 ya kura katika jimbo la South Carolina.Hillary Clinton amejinyukulia asilimia 27 na John Edwards amepata asilimia 18 tu.

Katika hotuba yake ya ushindi,Obama alisisitiza kuwa ukabila hauna umuhimu katika uchaguzi.Akaeleza kuwa uchaguzi huo unahusika na wakati wa kale na mustakabali na wala si mpambano kati ya matajiri na masikini,au vijana dhidi ya wazee na si suala la watu weusi dhidi ya weupe.

Amesema,chama cha Democratic kina msimamo mmoja,nao ni kukomesha kile alichokiita "sera za maafa" za serikali ya Bush.Ushindi huo katika jimbo la South Carolina ulikuwa muhimu sana kwa Obama ili kuweza kubakia katika kinyangányiro hicho,baada ya Clinton kujinyakulia ushindi katika majimbo ya Nevada na New Hampshire.Huo ni mpambano wa mwisho kwa chama cha Democratic kabla ya siku inayojulikana kama "Jumanne Kuu",katika kipindi cha siku kumi zijazo,ambapo zaidi ya majimbo 20 yatapiga kura katika uteuzi huo wa mwanzo.Wagombea wa chama cha Republican wanaendelea kufanya kampeni kwa mpambano wa Jumanne ijayo katika jimbo la Florida.