1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nyendo za maafisa wa kiraia wa Marekani nje ya eneo maalum za Baghdad zapigwa marufuku

Mohammed AbdulRahman19 Septemba 2007

Hatua hiyo inafuatia tukio la ufyatuaji risasi uliofanywa na walinzi wa kampuni ya ulinzi ya kimarekani “Blackwater”ambapo raia kadhaa wakiiraki waliuawa.

https://p.dw.com/p/CH82
Moshi ukitanda katika eneo la kijani"Green zone", baada ya moja wapo ya hujuma za wapiganaji.
Moshi ukitanda katika eneo la kijani"Green zone", baada ya moja wapo ya hujuma za wapiganaji.Picha: ap

Katika taarifa hii leo ambayo ilitumwa kwa Wamarekani walioko Irak, ubalozi wa Marekani mjini Baghadad umesema amri ya muda ya kupiga marufuku kusafiri kwa barabara nje ya eneo hilo imetolewa ili kuupitia upya utaratibu wa usalama.Kampuni ya Blackwater ni moja kati ya kampuni kubwa za kibinafsi za ulinzi nchini Irak, ikiulinda ubalozi wa Marekani.I rak imesema itazingatia upya shughuli za makampuni yote ya ulinzi baada ya ufyatuaji risasi wa walinzi wa Blackwater siku ya Jumapili mjini Baghdad ambapo watu 11 waliuawa.

Kwa upande wake ubalozi wa Marekani umesema kutokana na mkasa huo katika shughuli hizo za ulinzi, umeamuru kusitishwa nyendo zote za kiraia za wamarekani nje ya eneo hilo la kijani na kote nchini Irak. Ni katika eneo hilo ambako kuna ofisi za ubalozi wa marekani na nchi nyengine za magharibi wizara za serikali ya Irak.Tangazo hilo linakuja siku moja baada ya baraza la mawaziri la Irak kuiunga mkono hatua ya wizara ya ndani kusitisha leseni ya kampuni ya Blackwater na kuanzisha uchunguzi juu ya kilichotokea.

Wizara ya ulinzi ilisema walinzi wa kampuni hiyo walianza kufyatua risasi hovyo baada ya kombora kuangukia karibu na mlolongo wa magari waliokua wakiyasindikiza kwa ulinzi magharibi mwa Baghdad . Kampuni hiyo ilisema watumishi wake walichukua hatua muwafaka na inayofaa panapozuka hujuma. Hivi sasa serikali ya Irak na Marekani zimeunda kamati ya pamoja kuchunguza mauaji hayo. Maoni ya wairaki kuhusiana na makampuni ya ulinzi ambayo yamekuweko Irak tangu kuangushwa utawala wa Saddam Hussein 2003 ni kwamba walinzi hao wamegeuka kuwa sawa na jeshi la binafsi.

Wakati huo huo mbunge mmoja aliyekaribu na Waziri mkuu Nuri al-maliki, Sami al Askary amenukuliwa na gazeti la al-sabah akisema kwamba Bw al-Maliki atafanya mageuzi ya baraza lake la mawaziri hivi karibuni. Serikali yake ya mseto imekua ikikabiliwa na mzozo baada ya mawaziri kadhaa kutoka kundi la washia linalomuunga mkono kionozi Mukhtadar al-Sadr na wale kundi moaja la Wasunni kujitoa serikalini. Hatua hiyo imeiacha serikali hiyo ikiwa na Washia na Wakurdi pekee, Hadi sasa juhudi za kuondoa tafauti zilioko zimeshindwa kuzaa matunda.