1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu kukutana na Obama leo mjini Washington

Josephat Nyiro Charo6 Julai 2010

Rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa kukutana hii leo na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuzipiga jeki juhudi za kuanzisha mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Wapalestina

https://p.dw.com/p/OBVk
Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: AP

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kukaribishwa vizuri safari hii, kinyume kabisa na ilivyokuwa wakati alipoitembelea Marekani mnamo mwezi Machi mwaka huu, wakati ambapo rais Obama hakuonyesha kuwa na haja ya kukutana naye kwa sababu ya mgogoro kuhusu kupanuliwa kwa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi huko Jerusalem Mashariki.

Rais Obama anaitaka Israel irefushe marufuku ya ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi inayomalizika mwezi Septemba mwaka huu, lakini viongozi wa mrengo wa kulia nchini Israel, akiwemo waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo, Avigdor Lieberman, wanapinga vikali.

Rais Obama na makamu wake bwana Joe Biden, watakutana na Netanyahu wakati wa chakula cha mchana huko ikulu.

Joseph Biden und Benjamin Netanyahu
Makamu wa rais wa Marekani, Joe Biden(kushoto) na waziri mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: AP

Juhudi za kidiplomasia kabla ziara ya Netanyahu, yakiwemo mazungumzo kati ya waziri wa ulinzi wa Israel, Ehud Barak na waziri mkuu wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Salam Fayyad, zimeashiria hatua ya maendeleo katika mchakato wa kutafuta amani uliokwama.

Karata za kisiasa zimebadilika huku rais Obama akiwa na hamasa kuhusu umuhimu wa uhusiano baina ya Israel na Marekani huku uchaguzi wa bunge ukikaribia kufanyika nchini Marekani mwezi Novemba mwaka huu, na Netanyahu akionekana kuwa tayari kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Wapalestina.

Huku kukiwa hakutarajiwi kutolewa matangazo muhimu hii leo, maafisa wa Marekani wameelezea matumaini yao kuhusu uwezekano wa kupatikana ufanisi baada ya wiki kadhaa za juhudi za kidiplomasia zilizofanywa na mjumbe wa rais Obama katika Mashariki ya Kati, George Mitchell.

Wapalestina walisitisha mazungumzo ya ana kwa ana na Israel mnamo Desemba mwaka 2008 wakati Israel ilipofanya uvamizi wa siku 22 dhidi ya Ukanda wa Gaza unaotawaliwa na kundi la Hamas, kwa lengo la kukomesha mashambulio ya maroketi dhidi ya Israel.

Kwenye ajenda ya mkutano kati ya rais Obama na waziri mkuu Netanyahu ni azma ya Iran kutaka kutengeneza silaha za nyuklia na Ukanda wa Gaza. Israel imeregeza hatua yake ya kuuzingira ukanda huo kwa kuruhusu bidhaa za matumizi ambazo zilikuwa zimepigwa marufuku kwa miaka kadhaa. Hata hivyo, bidhaa muhimu za ujenzi hazitaruhusiwa, na marufuku ya usafiri na uuzaji wa bidhaa katika nchi za nje itaendelea, huku sheria mpya za Israel zikitarajiwa kutofanya lolote kuimarisha uchumi wa Gaza uliosambaratika.

Israel imechukua hatua hiyo kufuatia shinikizo lililosababishwa na uvamizi wa meli ya misaada iliyokuwa ikielekea Gaza, ambapo Waturuki 9 waliuwawa mmoja wao akiwa Mmarekani.

Israelischer Angriff auf Hilfskonvoi für Gaza
Picha inayoonyesha abiria aliyejeruhiwa kwenye meli ya misaada iliyovamiwa na IsraelPicha: AP

Uvamizi huo wa Mei 31 mwaka huu umevuruga uhusiano kati ya Israel na Uturuki, washirika wawili wa Marekani. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uturuki, Ahmet Davugtolu, ameonya kabla ya ziara ya Netanyahu mjini Washington, kwamba Uturuki itavunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Israel ikiwa haitaomba msamaha.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Marekani, Philip Crowley amesema anatarajia Netanyahu atamtarifu rais Obama kuhusu hatua za kwanza za uchunguzi wa Israel kuhusu mkasa wa kuvamiwa msafara wa meli za misaada na kujadiliana juu ya matukio mapya katika Ukanda wa Gaza.

Rais Obama anatarajiwa kumshinikiza Netanyahu kufanya mengi zaidi kuboresha hali katika Ukanda wa Gaza, ambayo amesema haiwezi kuendelea kubakia jinsi ilivyo. Israel imekuwa ikiuzingira ukanda huo tangu kundi la Hamas lilipoudhibiti mnamo mwaka 2007.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman