Ndege za Israel zaendelea kushambulia Ukanda wa Gaza
3 Januari 2009Rais Bush ameilaumu Hamas kwa hali iliyozuka hivi sasa kwenye Ukanda wa Gaza.Amesisitiza kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano hayawezi kupatikana mpaka Hamas itakapoacha kurusha maroketi dhidi ya Israel.
Hapo awali,mratibu mkuu wa misaada ya Umoja wa Mataifa kwa eneo hilo,Maxwell Gaylard alisema, maafa ya kibinadamu yanachomoza katika kanda hiyo,kwa sababu misaada ya chakula,dawa na mahitaji mengine imezuiliwa.Israel inashikilia kuwa bado kuna chakula na dawa za kutosha katika eneo la Gaza, licha ya operesheni yake ya kijeshi iliyoanzishwa kujibu mashambulizi ya roketi ya Hamas.Kwa mujibu wa maafisa wa Kipalestina,zaidi ya watu 420 wameuawa na wengine 2,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel ya siku saba mfululizo.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech,Ufaransa na Sweden wanatazamia kwenda Mashariki ya Kati siku ya Jumapili,huku zikiwepo ishara kuwa vikosi vya nchi kavu vya Israel vimekaa tayari kuvamia Ukanda wa Gaza.