1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi nyingi zimelaani hali ya hatari ya Pakistan

5 Novemba 2007

Mawakili nchini Pakistan wamefanya maandamano katika miji mbali mbali nchini humo kupinga hatua ya hali ya hatari iliyotangazwa na rais Pervez Musharraf wakati huo huo nchi mbali mbali zinaendelea kulaani hatua ya serikali ya Pakistan ya kutangaza hali ya hatari,hadi sasa zaidi ya 1,500 wamekamatwa.

https://p.dw.com/p/C77E
Kiongozi wa Pakistan Jenerali Pervez Musharraf
Kiongozi wa Pakistan Jenerali Pervez MusharrafPicha: AP

Maandamano makubwa kabisa yamefanyika katika miji ya Islamabad, Karachi Lahore, na Rawalpindi nchini Pakistan, kwa mara ya kwanza tangu rais Pervez Musharraf alipotangaza hali ya hatari siku ya jumamosi.

Polisi mjini Islamabad walitumia gesi za kutoa machozi na pia kuwapiga virungu mawakili wanaoandamana,

mawakili kadhaa wamejeruhiwa na mamia wamekamatwa katika maandamano yaliyofanyika nje ya mahakama katika miji mbalimbali nchini Pakistan.

Nchi kadhaa pia zimelaani hatua hiyo ya kutangazwa hali ya hatari na rais Musharraf.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Javed Cheema amefahamaisha kwamba watu zaidi ya 1,500 wamekamatwa tangu siku ya jumamosi na kwamba watu hao ni miongoni mwa wavunja sheria na pia ni miongoni mwa watu waliokiuka amri ya kutofanya mikutano.

Miongoni mwa nchi zinazopinga hatua ya uongozi wa Pakistan wa kuiweka nchi hiyo chini ya amri ya hali ya hatari ni Marekani ambayo imeitaka nchi hiyo kuitisha uchaguzi kwa wakati uliopangwa.

Marekani imesema kuwa ijapokuwa Pakistan ni nchi mshirika wake katika kupambana na kundi la kigaidi la Al Qaeda imelazimika kuahirisha mazungumzo muhimu ya usalama baina ya nchi hizo mbili.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates amesema kuwa Jenerali Musharraf anahitajika kuirejesha nchi yake katika hali inayozingatia katiba na wakati huo huo kuheshimu demokrasia.

Waziri wa ulinzi wa Marekani ameongeza kwa kusema kuwa nchi yake inachunguza upya mpango wake wa misaada kwa serikali ya Pakistan.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleeza Rice akiwa mjini Ramallah amemtolea mwito rais Pervez Musharraf wa Pakistan kuheshimu katiba ya nchi na kuitisha uchaguzi.

Kamishna mkuu wa wa umoja wa mataifa anaesimamia maswala ya haki za binadamu Louise Arbour ameelezea kutoridhika kwake na hatua ya utawala wa Pakistan.

Arbour amesema hali ya hatari ingepaswa tu kutangazwa kuambatana na vitisho vinavyoikabili nchi lakini sio kwa ajili kukandamiza hadhi na uhuru wa mahakama.

Mkuu huyo wa maswala haki za binadamu wa umoja wa mataifa ameelezea wasiwasi wake kufuatia ripoti kwamba majaji, mawakili, wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu wamekamatwa au wamezuiliwa majumbani mwao akiwemo Asma Jahangir muwakilishi maalum wa umoja wa mataifa anaeshunghulikia maswala ya dini na uhuru wa kuabudu.

Bibi Louise Arbour ameitaka Pakistan ieleze waziwazi hali ya watu waliokamatwa aidha kuhaikikisha kuwa mtu hakamatwi iwapo anafanya shughuli ambazo hazikiuki sheria za nchi.

Serikali ya Uholanzi imekatiza misaada ya maendeleo kwa Pakistan kuonyesha kuwa haiungi mkono hatua iliyochukuliwa na rais Pervez Musharraf.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uholanzi Francesco Mascini amesema hatua ya serikali yake inalenga kumshinikiza rais Musharraf arejeshe demokrasia nchini mwake na pia Uholanzi inamtaka rais Musharraf atoe ahadi kuwa uchaguzi wa Pakistan utafanyika kwa wakati uliopangiwa.

Naibu waziri wa maendeleo wa Uholanzi Bert Koenders ametangaza kuwa nchi yake imekatiza msaada wa Euro milioni 15 sawa na dola milioni 22 zilizopangiwa kusaidia mpango wa ellimu ambazo Pakistan ingezipokea kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Uholanzi pia ilikuwa na nia ya kuongeza msaada huo hadi kufikia dola milioni 40 katika kipindi cha mwaka ujao.

Wakati huo huo naibu waziri wa habari wa Pakistan Tariq Azeem amekanusha tetesi za awali zilizosema kuwa naibu amiri jeshi wa Pakistan amemzuia rais Pervez Musharraf ndani ya nyumba yake.