1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI:Wanadiplomasia wa kigeni wapewa onyo na serikali

1 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCWF

Serikali ya Kenya inawataka wanadiplomasia wa nchi za kigeni kutojihusisha na siasa za nchi hiyo wakati kampeni zinaendelea katika maandalizi ya uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Katika miaka ya hivi karibuni wanadiplomasia wamekuwa wakishinikiza serikali ya Rais Kibaki kwa madai ya vitenddo vya rushwa katika ngazi za juu.

Kwa mujibu wa naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Kenya Moses Wetangula,kipindi cha kampeni za uchaguzi husababisha mivutano ya kisiasa jambo ambalo ni la kawaida. Kiongozi huyo anatoa wito kwa wanadiplomasia hao kutojihusisha na siasa za nchi.

Wanadiplomasia hao kwa upande wao wanatoa wito wa wafanyikazi wa serikali kutopegemea upande wowote kufuatia agizo la Waziri wa Usalama wa Kitaifa John Michuki la kutaka uongozi wa mikoani kuunga mkono serikali katika kipindi hicho cha matayarisho ya uchaguzi.

Rais Kibaki kwa upande wake anatoa wito kwa viongozi wa kisiasa kutounga mkono vitendo vya uchochezi na badala yake kushirikiana ili kuimarisha umoja katika nchi.Rais Kibaki ametangaza nia yake ya kutaka kuwania wadhifa wa rais kwa muhula wa pili huku vyama vya upinzani vikitisha kuandamana na kususia uchaguzi endapo serikali haitakubali kufanya mabadiliko muhimu ya katiba.