1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musharraf akubaliana na kiongozi wa upinzani

Maja Dreyer29 Agosti 2007

Rais Musharraf wa Pakistan na waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Benazir Bhutto, aliyeko uhamishoni mjini London, Uingereza, wamekubaliana juu ya mpangaowa kugawa madaraka. Haya ni kulingana na Bi Bhutto aliyesema hivyo katika mahojiano yake na gazeti moja la Uingereza.

https://p.dw.com/p/CH8q
Benazir Bhutto, waziri mkuu wa zamani wa Pakistan
Benazir Bhutto, waziri mkuu wa zamani wa PakistanPicha: AP

Makubaliano haya kati ya rais Musharraf na kiongozi wa chama cha upingazi Bhutto aliyewahi kuwa waziri mkuu yamethibitishwa pia na waziri wa mambo ya reli na rafiki yake Musharraf, Sheikh Rashid akiongea mbele ya waandishi wa habari mjini Islamabad.

Viongozi hao wawili waliongea kwa muda mrefu jijini London na kuafikiana juu ya kufanywa uchaguzi huru na kufuta mashtaka ya rushwa dhidi ya Bhutto ambayo yalimlazimisha kukimbia nchini. Aidha Musharraf alikubali kuondosha haki ya rais kuvunja serikali na bunge kama alivyoeleza waziri Rashid ambaye alisema ni masuala machache tu yanayobakia lakini haya pia yatatatuliwa.

Katika mahojiano yake, Benazir Bhutto ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa kwanza wa kike nchini Pakistan, alitaja pia juu ya suala la rais Musharraf kuwa ni mwanajeshi na kusema kuwa jambo hili limepatanishwa bila ya kutoa habari zaidi. Musharraf ambaye ni jenerali wa jeshi aliyechukua madaraka katika mapinduzi ya mwaka 1999 na aliendelea kuwa ni mshirika wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi alitumia sana wadhifa wake wa kijeshi kuimarisha mamlaka yake.

Wakati huo huo, Musharraf anakabiliwa na changamoto nyingine kutoka mahakama kuu ya nchi hiyo ambayo imekubali kusikiliza kesi dhidi ya rais juu ya haki yake ya kuwa kiongozi wa jeshi.

Shtaka hilo limepelekwa mahakamani na Qazi Hussein Ahmed, mkuu wa jumuiya ya vyama vya kidini akidai kulingana na sheria za jeshi, muda wa Musharraf kushika cheo cha mkuu wa jeshi umekwisha mwaka 2001. Vile vile anadai haki ya Musharraf kuongoza jeshi imeisha mwaka 2003 pale Musharraf alifikisha umri wa miaka 60 ambao ni umri wa kila afisa wa jeshi la Pakistan kustaafu.

Waliopeleka shtaka hilo mahakamani walitiwa moyo na mamuzi mbali mbali ya mahakama hiyo dhidi ya serikali ikiwemo ruhusa kwa mpinzani muhimu na waziri wa zamani Nawaz Sharif kurudi Pakistan baada ya miaka sita uhamishoni.

Sharif ameshaarifu kuwa anapanga kurudi nchini mwake mnamo wiki mbili kuanzia leo kuongoza kampeini ya kumuondoa madarakani rais Musharaf, kama kaka yake Sharif, Shabaz Sharif alivyosema akiongea na wenzetu wa idhaa ya Kiurdu ya Redio Deutsche Welle: “Insha'allah tutarudi Pakistan kabla ya mwezi wa Ramadhan na kukaa pamoja na familia zetu katika mwezi huu wa mfungo.”

Nawaz Sharif pia alimkosoa kiongozi wa upinzani Benazir Bhutto kwa kuafikiana na rais Musharraf akikumbusha kuwa mawaziri wote wakuu wa zamani walikubali kutoshirikiana na dikteta wa kijeshi.

Musharraf aliarifu kuwa anataka kuchaguliwa tena kama rais akiwa bado mkuu wa majeshi. Bi Bhutto, awali, alimtaka Musharraf amhakikishie kwamba atajiuzulu kama mkuu wa jeshi kabla ya mwaka huu kuisha. Lakini kutokana na shinikizo kubwa dhidi ya Musharraf huko Pakistan na nguvu ya upinzani kukua, Bi Bhutto anaaminika sasa anamtaka Musharraf kutoa nguo zake za kijeshi kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi wa Septemba au Oktoba mwaka huu.