1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mubarak na Peres wakutana Sharm el Sheikh

23 Oktoba 2008

Mada kuu kati mazungumzo yao ni kubadilishana wafungwa kati ya Israel na Hamas.

https://p.dw.com/p/FfKH
Hosni Mubarak na Ehud BarakPicha: AP

Rais Hosni Mubarak wa Misri na Shimon Peres wa Israel ,wanakutana leo huko Sharm-el Sheikh, nchini Misri kuzungumzia utaratibu wa amani wa Mashariki ya kati na juhudi inazofanya Misri kuandaa mabadilishano ya wafungwa kati ya Israel na chama cha Hamas.

Mazungumzo haya pia yanafanyika katika hali kuwa uchumi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, unaathirika mno kwa ukosefu wa raslimali ikitokana hali hii zaidi na vikwazo Israel ilivyowawekea wapalestina katika nyendo zao.Na hii licha ya kuongezeka misaada ya Banki kuu ya dunia.

Rais wa Israel tofauti na rais Mubarak wa Misri, hana madaraka ya utendaji,atapewa makaribisho kamili ya kiserikali. Marais hawa wawili watazungumza uhusiano kati ya nchi zao 2 jirani ambazo zilifunga mapatano ya kwanza ya amani kati ya nchi ya kiarabu na Israel hapo 1979.

Mazungumzo yao yamkini pia yakatuwama juu ya juhudi za Misri kupatanisha mpango wa kubadilishana mfungwa baina ya Israel na chama cha Hamas cha wapalestina kinachotawala Mwambao wa Gaza ili kumkomboa mwanajeshi wa Israel Gilad Shalit.Shalit alinyakuliwa katika hujuma kali iliofanywa Juni, 2006.

Misri miezi ya karibuni, ikichukua jukumu kubwa kupatanisha baina ya chama cha Hamas ambacho hakiitambui Israel na Israel ambayo pamoja na mshirika wake Marekani na Umoja wa Ulaya , imekitumbukiza katika orodha ya vyama vya kigaidi.

Chama cha Hamas kinadai kuwa Israel iwaache huru wafungwa 1,400 wa kipalestina pamoja na mamia waliohusishwa na mashambulio yaliongoza vifo vya waisraeli.

Israel na Hamas, ziliridhia upatanishi wa Misri kusimamisha mapigano kati yao huko Gaza hapo Juni 19 na hivyo kukomesha mapigano yaliodumu miezi kadhaa.

Ingawa pande zote mbili kwa kadiri kubwa zimeyaheshimu mapatano hayo,hakuna maendeleo makubwa yaliofikiwa kwenye mazungumzo ya kubadilishana wafungwa.

Israel inaendelea kukataa kuwaacha huru wafungwa wengi namna hiyo kama inavyodai Hamas.Wiki iliopita lakini, rais Peres wa Israel alisema mazungumzo ya moja kwa moja yameanzishwa tena.

Marais hao 2 wanatazamiwa pia kuzungumzia hali ya mazungumzo ya amani yanayoungwamkono na Marekani kati yaisrael na Palestina .Mazungumzo hayo yalifufuliwa tena hapo Novemba mwaka jana ikiwekwa shabaha kuu ya kufikia suluhisho hadi mwisho wa mwaka huu.Mazungumzo haya yamesita kabisa wiki chache zilizopita kufuatia kujiuzulu kwa waziri mkuu Olmert wa Israel huku waziri wake wa nje Livni, akijaribu sasa kuunda serikali mpya ili kujaza pengo analoacha Ehud Olmert.