1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji wa sinagogi Halle apandishwa kizimbani

Admin.WagnerD21 Julai 2020

Mwanamume mmoja raia wa Ujerumani anapandishwa kizimbani Jumanne (21.07.2020) kwa mauaji ya umwagaji damu yaliyowalenga wayahudi katika mji wa Halle, mashariki mwa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/3fdfr
Deutschland Prozess zum Terroranschlag von Halle
Picha: picture-alliance/dpa/H. Schmidt

Stephen B, mwenye umri wa miaka 28 anashitakiwa kwa kuwapiga risasi na kuwaua watu wawili mnamo mwezi Oktoba mwaka uliopita baada ya kujaribu na kushindwa kungia katika sinagogi mjini Halle. Ameshitakiwa kwa makosa mawili ya mauaji na anakabiliwa na mashitaka mengine ya jaribio la kuua.

Waendesha mashitaka wanasema Stephen alitumia vilipuzi na silaha kujaribu kuingia katika sinagogi hilo, ambamo waumini 52 walikuwa wakisherehekea sikukuu ya Yom Kippur, siku takatifu kabisa katika kalenda ya Wayahudi. Baada ya kushindwa kuuvunja mlango wa mbao wa sinagogi hilo uliokuwa umefungwa, alimpiga risasi na kumuua mwanamke mmoja mpita njia na mwanamume mmoja katika duka la kebabu lililo karibu.

Mshambuliaji huyo aliurekodi uvamizi huo na kuupeperusha moja kwa moja kwenye mtandao wa mawasiliano wa intaneti. Shambulizi hilo liliishutua Ujerumani na kuchochea wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa machafuko ya watu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na machafuko dhidi ya wayahudi, miaka 75 tangu kumalizika kwa enzi ya utawala wa manazi wa Ujerumani.

Mshukiwa amekiri na kuonyesha malengo yake

Waendesha mashitaka wamesema Stephen alitoa ushahidi akikiri na kuthibitisha malengo ya msimamo mkali wa mrengo wa kulia na chuki dhidi ya wayahudi. Stephen pia alichapisha nyaraka mtandanoni kutoa wito wayahudi wote wauawe. Video yake itaonyeshwa mahakamani. Anakabiliwa na mashitaka mengine ya uchochezi wa chuki kwa kukana mauji ya wayahudi Holocaust katika video hiyo.

Kesi yake inasikilizwa katika mahakama ya wilaya ya Magdeburg na imepangwa kuendelea hadi katikati ya mwezi Oktoba mwaka huu. Henning Haberland, msemaji wa mahakama ya Magdeburg, alisema, "Kwa mujibu wa mashitaka, mshtakiwa anadaiwa aliyashambulia maadili ya msingi ya jamii yetu, yanayojumuisha kuishi kwa amani kwa makundi mbalimbali ya kijamii. Anadaiwa hasa kusababisha uchungu na mateso binafsi yasiyo kifani. Sheria itachukua mkondo wake na kesi yake itaendeshwa kwa haki."

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa katika jarida la Spiegel la hapa Ujerumani, tathmini ya kisaikolojia aliyofanyiwa Stephen ilibaini kuwa ana matatizo ya kitabia na dalili za ugonjwa wa akili wa tawahudi au usonji. Ripoti hiyo iliongeza kusema hata hivyo, alionekana anafahamu fika kuhusu matendo yake na hawezi kusamehewa asiwajibishwe.

Iwapo atatiwa hatiani Baillet huenda akafungwa maisha jela.

(dpae, dpae)