1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huzuni, ghadhabu vyagubika mauaji ya Hanau

Lilian Mtono
21 Februari 2020

Maelfu ya watu wamekusanyika kwenye miji kadhaa ya nchini Ujerumani kuonyesha mshikamano kwa wahanga wa shambulizi la bunduki lenye viashiria vya ubaguzi wa rangi katika mji wa Hanau.

https://p.dw.com/p/3Y7MK
Hanau Trauer um Opfer nach Amoklauf
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Ni hatua inayokuja katika wakati ambapo kuna ongezeko la miito ya mamlaka kuchukua hatua kali dhidi ya watu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia. 

Katika mji wa Halle, takriban watu 350 walionyesha mshikamano na kuungana pamoja na jamaa wa wahanga wa shambulizi hilo la Hanau kwa kukaa kimya kwa dakika moja katika mkutano wa hadhara hapo jana. Shambulizi hilo kwenye mji wa Hanau ulioko magharibi mwa Ujerumani limekuja miezi minne baada ya mfuasi mmoja wa mrengo mkali wa kulia kuwaua zaidi ya watu 50 waliokuwa kwenye sinagogi mjini Halle.

Rais wa shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amelaani mashambulizi hayo akiyataja kama kitendo kibaya kabisa cha kigaidi, kinachokumbusha mengi yanayofanana na hilo.

Meya wa Hanau Claus Kaminsky kwenye kusanyiko la watu takriban 2,000 la kuwakumbuka wahanga hao hapo jana alisema hii siku itakuwa moja ya siku mbaya kabisa kihistoria.

Hanau Trauer um Opfer nach Amoklauf
Miongoni mwa waombolezaji waliobeba picha za jamaa zao waliouawa kwenye shambulizi la HanauPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

"Tangu saa nne jana usiku, sio tu Hanau na familia za wahanga, bali ulimwengu hauko tena sawa na ulivyokuwa awali. Mapendwa raia wenzangu, nyakati na siku kama hii vitakuwa miongoni mwa siku mbaya kabisa katika historia ya jiji letu.", alisema meya huyo.

Mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Tobias Rathjen aliyekuwa na silaha aliwashambulia kwa risasi watu tisa wenye historia ya uhamiaji katika makazi ya Hanau yaliyoko Frankfurt siku ya Jumatano kabla ya kumuua mama yake na kisha kujiua.

Rais wa Romania Klaus Lohannis ameandika kwenye ukurasa wa twitter kwamba raia mmoja wa taifa hilo pia amekufa kwenye shambulizi hilo.

Shambulizi la Hanau linalofanywa katika wakati ambapo kuna ongezeko la wasiwasi kuhusu misimamo mikali ya mrengo wa kulia ikijionyesha dhahiri kufuatia mashambuli ya awali pamoja na kuibuka kwa chama kinachopinga vikali wageni cha Mbadala wa Ujerumani ama Alternative for Germany, AfD.

20.02.2020 Matangazo Ya Mchana

Afisa wa ngazi za juu wa chama cha Social Democratic, ambacho ni mshirika mdogo kwenye serikali ya shirikisho la kansela Angela Merkel Lars Klingbeil alipozungumza na shirika la habari la hapa Ujerumani, ARD amekituhumu chama cha AfD kwa kile alichosema kinatoa maudhui ya kiitikadi kwa watu kama mshambuliaji huyo wa Hanau.

Ingawa chama hicho kinakana kuhusika na mashambulizi hayo ya itikadi kali, lakini tayari kimeanza kuchunguzwa na shirika na kijasusi la ndani la Ujerumani.

Gazeti la kila siku la Ujerumani la Frankfurter Rundschau kwenye uhariri wake hii leo limeandika ni muhimu hatimaye kutambua kwamba itikadi kali za mrengo wa kulia ni kitisho halisi na kikubwa kinachowakabili watu wa taifa hili na kinachotakiwa sasa ni hatua kali dhidi ya kitisho hicho.