1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kuinua maendeleo ya kiuchumi Afrika Magazetini

Oumilkheir Hamidou
7 Julai 2017

Misaada ya maendeleo na ila zake, jinsi mataifa matano ya Sahel yanavyopania kuwashinda nguvu magaidi na wahalifu na juhudi za Umoja wa ulaya za kujipunguzia kishindo kinachotokana na mikururo ya wakimbizi magazetini

https://p.dw.com/p/2g8Zz
G20 Gipfel in Hamburg | Conde & Jinping & Zuma
Picha: Reuters/J. MacDougall

 

Tunaanza na misaada ya maendeleo na ila zake. "Ajira, elimu na afya ndiyo kipimo" linaandika gazeti la mjini Berlin, Berliner Zeitung. Gazeti linasema kawaida katika kutolewa misaada ya maendeleo "walioendelea" ndio wanaowaarifu wale ambao "hawakuendelea" kuhusu kile wanachokihitaji ili kufikia maendeleo. Hiyo ndiyo sababu nguzo ya ushirikiano kati ya nchi za kaskazini na zile za kusini imelemaa, tukiweka kando rushwa, tabia ya kutegemea ruzuku na kuchoshwa kwa wafadhili. Gazeti la Berliner Zeitung linahisi mpango wa kuhimiza maendeleo barani Afrika, uliopendekezwa na serikali kuu ya Ujerumani na kuorodheshwa katika ajenda ya mkutano wa kilele wa mataifa 20 yaliyoendelea na yale yanayoinukia kiuchumi, G-20 uliomalizika jana mjini Hamburg- "Compact with Africa", mpango unaohimiza zaidi vitega uchumi vya kibinafsi ndio fursa halisi itakayoweza kuyasaidia mataifa ya ulimwengu wa tatu kujiendeleza.

Nafasi za kazi ndio kipaumbele

Hata kama mpango huo umeandaliwa katika nchi ya kaskazini, na kwamba suala la waafrika wenyewe wanayaangalia vipi maendeleo yao halijapewa umuhimu mkubwa, hata hivyo Berliner Zeitung linahisi fikra jumla ya kulenga maendeleo ya Afrika kupitia vitega uchumi vya kibinafsi ni fikra inayolingana na matakwa ya waafrika. Uchunguzi wa maoni ya wananchi uliosimamiwa na taasisi ya  "Afrobarometer", muda mfupi kabla ya mkutano wa G-20 kuanza, umeonyesha asilimia 38 ya walioulizwa maoni yao kuhusu wapi vitega uchumi vya kibinafsi viwekezwe, wanahisi katika miradi ya kubuni nafasi za kazi huku asilimia 32 wakizitaja huduma za afya ndio kipaumbele na aslimia 24 wakitanguliza mbele umuhimu mkubwa zaidi kwa elimu. Berliner Zeitung limemaliza kwa kusema asilimia 55 ya waafrika wangependelea kuziona serikali za nchi zao zikiwajibike zaidi katika sekta ya elimu, huku asili mia 51 wakitanguliza mbele huduma za afya.

Kituo cha kuwaokoa wakimbizi kujengwa Libya

Mojawapo ya malengo ya mpango wa kuhimiza maendeleo ya kiuchumi barani Afrika, "Compact with Afrika" ni kusaidia kuwapatia matumaini mema vijana na kwa namna hiyo kuondokana na fikra ya kutaka kuelekea Ulaya. Gazeti la die tageszeitung linachambua juhudi za Umoja wa Ulaya zilizolengwa kuishurutisha Libya iahidi kuwaokoa wakimbizi katika bahari ya kati na kuwarejesha nchini humo, baada ya Italia kudai ipunguziwe mzigo wa wakimbizi wanaoingia nchini la sivyo itazizuwia meli za mashirika yasiyomilikiwa na serikali zisitie nanga katika bandari za nchi hiyo. Baada ya masharti ya Italia kukataliwa na Ufaransa na Uhispania na kufuatia mkutano wa dharura kati ya Ufaransa na Ujerumani kuhusu suala hilo, halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imetangaza mkakati unaozungumzia dhamiri ya Umoja wa Ulaya ya kuzidi kuwasaidia viongozi wa Libya. Mjini Brussels viongozi wanazungumzia kuhusu uwezekano wa kutoletwa Italia wakimbizi watakaookolewa katika bahari ya Mediterania na badala yake watakuwa wakirejeshwa Libya. Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya inataka kusaidia kujenga kituo cha opereshini za kuwaokoa wakimbizi katika bahari ya Mediterenia nchini Libya. Libya itapatiwa msaada wa Euro milioni 45 ili kuimarisha ulinzi wa mpakani. Die Tageszeietung linamaliza kwa kuandika hadi mradi huo utakapokamilika mzigo wa wakimbizi utaendelea kuilemaza Italia.

Umoja wa Ulaya kuchangia katika juhudi za kupambana na ugaidi katika eneo la Sahel

Mada yetu ya mwisho magazetini inagusia pia ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na mataifa ya Afrika, safari hii lakini ni ushirikiano pamoja na mataifa matano ya kile kinachojulikana kama nchi za ukanda wa Sahel, Burkina Faso, Mali, Mauritania, Niger na Chad. Viongozi wa nchi hizo wametiliana saini mapema mwaka huu makubaliano ya kuunda kikosi cha pamoja kupambana na ugaidi na dhidi ya makundi yote yanayofanya biashara kinyume na sheria. Umoja wa Ulaya linaandika Frankfurter Allgemeine umeahidi kutoa Euro milioni 50 kusaidia juhudi hizo. Msaada huo ni ushahidi timamu kwa Afrika na jumuiya ya kimataifa linaandika Frankfurter Allgemeine, linalomaliza kwa kusema Ulaya na Afrika wanakabiliana na changamoto sawa na fursa ya kuibuka na ushindi dhidi ya visa hivyo.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSEM/ALL

Mhariri:Josephat Charo