Mkutano wa Munich wazilaani China na Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.02.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa Munich wazilaani China na Urusi

China na Urusi zimendelea kushutumiwa vikali kwa kutumia kura ya turufu kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kumaliza ghasia nchini Syria, ambako mauaji dhidi ya waandamanaji yanaripotiwa kuendelea.

Mkutano wa usalama mjini Munich, Ujerumani.

Mkutano wa usalama mjini Munich, Ujerumani.

Mwanaharakati wa vuguvugu la mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Nobel, Tawakkul Karman, ameulaani vikali utawala wa Bashar al-Assad. Mtetezi huyo wa mageuzi kutoka Yemen anayehudhuria mkutano wa usalama unaofanyika Munich, Ujerumani, pia alizitaka nchi za Kiarabu kuwafurusha mabalozi wa Syria ili kuonesha ghadhabu yao kuhusiana na ukandamizaji unaoendelea kufanywa na serikali dhidi ya wanaounga mkono demokrasia nchini Syria.

Wito huo uliungwa mkono na Waziri Mkuu wa Tunisia, Hamadi Jebali, ambaye serikali yake ilichukua uamuzi huo hapo awali. Alisema watu wa Syria hawataraji kusikia taarifa ndefu kutoka kwao pamoja na shutuma isipokuwa wanataraji kuona vitendo.

Tunisia, ambako vuguvugu la wimbi la mageuzi lilianzia, imekuwa katika mstari wa mbele kuupinga utawala wa Rais al-Assad. Mazungumzo hayo ya usalama mjini Munich yanafanyika siku moja baada ya taarifa za watu 260 kuuwawa na vikosi vya usalama katika mji wa kati wa Homs kwenye ukandamizaji unaoendelea wa serikali.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov.

Hapo Jumamosi (04.02.2012) Urusi na China zilitumia kura ya turufu kulipinga azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, rasimu ambayo imeungwa mkono na nchi nyingi za Kiarabu na za Magharibi.

Naye Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Qatar, Khalid al-Attiyah, alisema kushindwa kulipitsha azimio hilo kunaipa leseni Syria kuendelea kuwauwa waandamanaji. Qatar ndiyo iliyokuwa nchi ya pekee ya Kiarabu iliyotoa mchango wa kijeshi kwa amri ya kutoruka kwa ndege dhidi ya Libya, hatua iliyosaidia kuondolewa madarakani aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo marehemu Muammar Gaddafi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davotuglu, alidokeza kuwa baada ya duru kadhaa za mazungumzo baina ya nchi za kanda na Syria, na kisha hatua ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, matumaini yaliyosalia yalikuwa Umoja wa Mataifa kutoa mwongozo.

Wakati huo huo, nchi za Kiarabu zimeahidi kuendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi kuhusu mzozo wa Syria, ijapokuwa jaribio lao la kutafuta uungaji mkono kutoka kwa Umoja wa Mataifa zilizuiwa na Urusi na China.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davutoglu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davutoglu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Nabil El-Araby, amesema hatua ya Urusi na China haimaanishi kuwa jamii ya kimataifa haiungi mkono azimio la Jumuiya hiyo ya Kiarabu.

Na huku hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, atafanya ziara nchini Syria wiki hii ambako atamtaka rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad atekeleze mageuzi muhimu na ya haraka. Katika ziara ya hapo Jumanne (07.02.2012), Lavrov ataandamana na mkuu wa kitengo kinachoshughulikia ujasusi wa nje.

Ziara hii inakuja baada ya Urusi kuzighadhabisha nchi za magharibi na wapinzani nchini Syria kwa kupiga kura ya turufu dhidi ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalolaani ukandamizaji wa Assad dhidi ya waandamanaji.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa Urusi inahofia kuondoka kwa Assad kutaigharimu Urusi mamia ya mamilioni ya dola katika mikataba ya silaha, pamoja na mshirika wake wa mwisho aliyesalia katika eneo hilo baada ya kuangushwa kwa Muammar Gaddafi kupitia wimbi la mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu lililoanzia Tunisia mapema 2011.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/DPA

Mhariri: Mjahid, Amina

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com