Mkutano wa kimataifa juu ya HIV na Ukimwi waanza leo New York
7 Juni 2011Mkutano huo wa kilele unaoanza leo unategemewa kupitisha uamuzi juu ya ni watu wangapi duniani watapata nafasi ya kupokea matibabu maalum ya kupunguza makali ya maradhi hayo yaliyokwisha sababisha vifo vya kiasi watu millioni 30 katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.
Viongozi wakuu 30 wa dola na serikali zitakazotoa fedha za kugharimia mpango huo watajadiliana kwa kina juu ya kiasi gani cha watu wanaostahili kupewa dawa na matibabu maalum ambayo kwa mujibu wa utafiti mpya imeonyesha ni utaratibu unaoweza kupunguza kwa kiwango kikubwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Kundi la madaktari wasiokuwa na mipaka la Medicins Sans Frontieres limeutaka mkutano huo kuwafikiria watu millioni 9 katika mpango huo wa matibabu ya Ukimwi katika kipindi cha miaka 4 ijayo pendekezo ambalo linakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wachangiaji kadhaa muhimu wa fedha katika mpango huo. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa watu millini 34 wanakadiriwa kuishi na virusi vya Ukimwi na wengine zaidi ya millioni 9 hawapati matibabu.
Wanadiplomasia wanasema kwamba majadiliano juu ya idadi ya wanaopaswa kupokea matibabu hayo katika nchi mbali mbali ambayo yanaweza kubadili kabisa gharama kwa mamilioni ya dolla yamekuwa yakiendelea tangu hata kabla ya mkutano wa leo.
Hata hivyo wataalamu na wanaharakati wa kupambana na maradhi ya Ukimwi wanasema kwamba itakuwa hakuna maana ikiwa nchi wafadhili wa mpango huo dhidi ya kuenea kwa Ukimwi hawatokuwa tayari kutoa fedha zinazohitajika wakati kunahitajika hatua madhubuti za kungo'a kabisa shina la janga hilo.
Shirika la UNAIDS linasema kwamba kunahitajika billioni 6 zaidi kila mwaka kuepusha vifo vya watu millioni 7 kufikia mwaka 2020.Fedha hizo zitatumika kununua madawa yanayoweza kupunguza idadi ya kila mwaka ya maambukizi mapya kutoka watu millioni 2 .5 mwaka 2009 hadi watu millioni 1 kufikia mwaka 2015.
Aidha makundi ya wataalamu wa afya yanasema kwamba serikali za dunia zinabidi kuchukua hatua ya kupunguza gharama za madawa.
Mwandishi Saumu MwasimbaAFPE
Mhariri AbdulRahman.