1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri kwenye mkwamo

7 Februari 2011

Baraza jipya la mawaziri wa Rais Hosni Mubarak limekutana leo hii, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuundwa kwake wiki iliyopita, na ikiwa bado waandamanaji wanaendelea na madai yao ya kumtaka Mubarak aijuzulu haraka.

https://p.dw.com/p/10CRj
Waandamanaji mjini Alexandria
Waandamanaji mjini AlexandriaPicha: dapd

Misri imekwama. Leo nzima imepita kukiwa hakuna hata upande mmoja uliopiga hatua ya maana kuelekea kwenye suluhu, zaidi ya hatua ya serikali kupunguza muda wa amri ya kutotoka nje nyakati za usiku, ambapo sasa inaanza saa mbili usiku, badala ya saa moja.

Hata hivyo, tangu amri hii kuwekwa hapo Januari 28, haijawahi kuheshimiwa na waandamanaji. Waandamanaji wameendelea na mkusanyiko wao katika uwanja wa Tahrir na katika mji mkuu wa Cairo na miji mingine ya nchi hiyo, na dai lile lile la Rais Mubarak kuondoka.

Naye Rais Mubarak, hata baada ya kikao cha kwanza cha baraza lake jipya la mawaziri cha leo hii, hajabadilisha msimamo wake wa kuendelea kubakia madarakani hadi hapo mwezi Septemba.

Waandamanaji wakataa kuondoka

Waandamanaji wametanda Tahrir
Waandamanaji wametanda TahrirPicha: picture-alliance/dpa

Mazungumzo ya jana kati ya serikali, ikiwakilishwa na Makamo wa Rais Omar Suleiman, na waandamanaji wakiwakilishwa na makundi kadhaa ya upinzani, hayakuweza kuwaondoa waandamanaji mitaani.

Badala yake wameapa kuendeleza kampeni yao mitaani kwa maandamano makubwa zaidi hapo kesho na Ijumaa. Hii ni licha ya Suleiman kufikia makubaliano na upinzani wa kuunda kamati pamoja kusimamia mchakato wa kubadilisha katiba ili kuruhusu uchaguzi na mageuzi mengine muhimu.

Gigi Ibrahim, ni mmoja wa waandamanaji, anayepingana kabisa na wazo la kuzungumza na serikali, akitaka maandamano yaendelee hadi mwisho wa njia.

"Hapa hakuna cha makubaliano. Watu wamekufa. Wengine bado wanashikiliwa na polisi. Waandishi wa habari wanasumbuliwa. Na matakwa yetu yako wazi kabisa: kuondoka kwa utawala, kuvunjwa kwa bunge na uchaguzi huru na wa haki na serikali ya kipindi cha mpito." Anasema Gigi.

Rais Mubarak, mwenye miaka 82, amekataa kabisa kumaliza utawala wake wa miaka 30, hadi hapo kura ya mwezi Septemba mwaka huu.

Mwanadamanaji mmoja alionekana kwenye uwanja wa Tahrir akiwa amebeba bango linalomwambia Mubarak, kwamba: Ulichoshindwa kukifanya kwa miaka 30, huwezi kukifanya kwa miezi sita. Ondoka!"

Je, maandamano yatosha?

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary ClintonPicha: AP

Kwa upande mwengine, maoni kutoka nchi za Magharibi, hasa Marekani, yanaonekana kubadilikabadilika ndani ya wiki hizi mbili za maandamano. Kuna ambao wanaona kuwa, tayari Mubarak ameshajitolea sana kwa madai ya waandamanaji.

Kwa mfano, amekubali kutogombea tena, amemuondoa kabisa mwanawe Gamal kwenye uwezekano wa kuwa rais ajaye, amemteua makamo wa rais kwa mara ya mwanzo tangu ainge madarakani miongo mitatu iliyopita, uongozi wa chama chake umevunjika na akalifuta kazi baraza lake la mawaziri.

Lakini kuna pia wanaoona kuwa, Mubarak amekuwa mgumu wa kuelewa hisia za waandamanaji, ambao hawataridhika mpaka yeye mwenyewe ang'oke.

"Anapaswa kuwachia madaraka. Maana imeshathibitika kuwa madaraka yake yamepoteza uhalali, na analazimika kuwajibika kisiasa kwa kukaa kando." Anasema kiongozi wa upinzani, Mohammed El-Baradei.

Wakati huo huo waandamanaji wanaendelea na maandamano yao kwenye uwanja wa Tahrir kudai Mubarak aondoke madarakani hivi sasa. Na leo walishiriki katika mazishi ya mwandishi wa habari Ahmed Mahmoud aliyeuawa hapo juzi, wakimtaja kuwa miongoni mwa mashujaa wa vuguvugu hili la mabadiliko.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman