1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka kumi ya kamisheni ya ukweli na suluhu

Räther, Frank 28 Oktoba 2008

Jee juhudi za kuponyesha kiwewe kilichosababishwa na sera za zamani za ubaguzi wa rangi na mtengano nchini Afrika zimefikia wapi?

https://p.dw.com/p/Fj3h
Rais mstaafu wa Afrika kusini Nelson MandelaPicha: AP


Miaka kumi imepita tangu kamisheni ya ukweli na suluhu ilipokamilisha shughuli zake nchini Afrika kusini.Lengo lake lilikua kufichua maovu yaliyofanywa wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi na mtengano-Apartheid na kuleta suluhu miongoni mwa wakaazi wa nchi hiyo.Lengo hilo lakini halikufikiwa kikamilifu.


Miaka kumi iliyopita,askofu mkuu Desmond Tutu alimkabidhi rais wa wakati ule Nelson Mandela madaftari matano yaliyosheheni jumla ya kurasa elfu tatu na mia tano.Kilichoratibiwa ndani ya madaftari hayo ni matokeo ya shughuli za miaka kadhaa za kimisheni ya ukweli na suluhu  za kufichua maovu na madhila yaliyofanywa katika enzi za ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid  pamoja na kujua chanzo cha hali hiyo.Waliokubali kuzungumzia yaliyotokea,walisamehewa.


Ni jukumu kubwa kupita kiasi,alisema wakati ule askofu mkuu Desmond Tutu:


"Tulikua na jukumu la kutafakari ukurasa mweusi wa historia yetu,ili kusaidia kutuliza huzuni na kiwewe miongoni mwa wananchi.Kwasababu,sisi sote nchini Afrika kusini tumeathirika.Hivyo ndivyo tunavyotaka kufikia umoja wa taifa na suluhu."


Lilikua jaribio la aina pekee kuwahi kushuhudiwa ulimwenguni wakati ule.Ukweli ulibainika japo kama si wote.Lakini lengo la kufikia suluhu kati ya weusi na weupe,kuundwa taifa la mchanganyiko wa makabila,au kama Tutu alivyokua akisema taifa la upinde....lengo hilo halikufikiwa.Kwasababu Nelson Mandela alifuatiwa madarakani na Thabo Mbeki, kama rais wa nchi hiyo mnamo mwaka 1999.Na hakufuata nyayo za Mandela za watu kuishi pamoja kwa masilahi ya pamoja ya nchi yao,bali aliwapendelea zaidi weusi.Ukawa mkondo wa nyeusi na nyeupe badala ya mkondo wa upinde.Hapakupita miaka mingi wataalam wenye asili ya kizungu,waliokua na maarifa ya muda mrefu,wakaanza kupokonywa vyeo walivyokua navyo.Hata vijana weupe waliomaliza masomo katika vyuo vikuu,wakajikuta bila ya matumaini ya kupanda daraja.Wakati huo huo lakini utawala wa Mbeki haukusaidia kuinua elimu miongoni mwa vijana weusi wa Afrika kusini.Ndio maana utakuta maafisa wengi hawana ujuzi lakini wao ndio wenye usemi..analalamika mfanyabiashara mmoja wa kijerumani Claas Daun



"Kinachokosekana ni mfumo madhubuti wa elimu kama ule tulio nao nchini Ujerumani.Nchi ni sawa na kampuni:ikiwa huna watu wa kutosha wenye ujuzi na maarifa,ikiwa hakuna ushirikiano,basi kampuni nalo litarejea nyuma."


Ukosefu wa ujuzi na maarifa ndio chanzo cha kuvurugika shughuli nyingi za idara za serikali.Sekta ya elimu na afya zimeporomoka.Na ingawa nyumba milioni kadhaa zimejengwa na mamilioni wamepatiwa umeme na maji safi pamoja na wegi miongoni mwa watu wasiojimudu kupatiwa huduma za jamii,bado kuna mengi ya kufanya.


Watu zaidi na zaidi wameanza kuvunjika moyo na wegine kufika hadi ya kuteremka majiani katika baadhi ya miji.

Hata chama cha ANC kimegawika tangu njama iliyopelekea kumng'owa madarakani Thabo Mbeki.Kuna hofu za kuripuka machafuko uchaguzi utakapoitishwa mwakani.


Na ikiwa hofu hizo zitathibitika basi madhara yake yanaweza kuziathiri pia fainali za komble la dunia la kabumbu mwaka 2010 ambazo lengo lake ni kuitembeza Afrika kusini mpya."