1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 ya uhusiano mpya kati ya Ufaransa na Ujerumani

8 Julai 2012

Kansela Angela Merkel na Rais Francois Hollande, siku ya Jumapili walikutana katika mji wa Rheims nchini Ufaransa, kukumbuka kuanzishwa upya kwa uhusiano baina ya mataifa hayo, baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

https://p.dw.com/p/15Tjt
Rais wa Ufaransa, Charles de Gaulle, na Kansela wa Ujerumani Konrad Andenauer wakisaini makubaliano ya ushirikiano mpya Julai 8, 1962.
Rais wa Ufaransa, Charles de Gaulle, na Kansela wa Ujerumani Konrad Andenauer wakisaini makubaliano ya ushirikiano mpya Julai 8, 1962.Picha: picture-alliance/dpa

Merkel na Hollande walishiriki ibaada ya misa katika kanisa la Rheims, kusherehekea siku ambapo nchi hizo zilifikia usuluhishi, Juni 8, 1962. Mkataba wa urafiki mpya ulisainiwa kati ya Rais wa Ufarasa wa wakati huo, Charles de Gaulle, na Kansela wa Ujerumani Konrad Adenauer.

Hollande na Merkel walivumilia hali mbaya ya hewa, na kukutana na umati wa watu waliokusanyika karibu na kanisa la Rheims. Baadaye walizindua bamba la usuluhisho, lilioandikwa kwa lugha ya Kijerumani, na kuwekwa sambamba na lile lililoandikwa kwa Kifaransa wakati wa sherehe ya kwanza.

Kansela Angela Merkel na rais Francoise Hollande wakisikiliza nyimbo za mataifa hayo wakati wa sherehe hiyo mjini Rheims, Ufaransa, Jumapili.
Kansela Angela Merkel na rais Francoise Hollande wakisikiliza nyimbo za mataifa hayo wakati wa sherehe hiyo mjini Rheims, Ufaransa, Jumapili.Picha: picture-alliance/dpa

Makubaliano hayo ya Julai 8, 1962 ndiyo yalitojenga msingi wa uhusiano baina ya Ufaransa na Ujerumani hadi kufikia sasa.. Baada ya misa, Merkel na Hollande walitoa hotuba kila mmoja nje ya Kanisa. Hollande alisema Adenauer na De Gaulle walisafisha njia ya mafanikio kama vile soko la pamoja, kuungana upya kwa Ujerumani na kuanzishwa kwa sarafu ya pamoja ya euro.

Merkel ataka Ulaya ishikamane kukabiliana na hali ngumu
Kwa upande wake, Kansela Merkel aliwapengeza viongozi hao wawili kwa kusaidia kusanifu uhusiano mpya baina ya Ufaransa na Ujerumani na Ulaya kwa ujumla. "Walifungua ukurasa mpya," alisema Merkel kabla ya kuwataka wakaazi wa Ulaya kuonyesha mshikamano wakati huu wa mgogoro wa kifedha unaozikabili nchi zinazotumia sarafu ya euro barani Ulaya.

Merkel, aliyekulia Ujerumani Mashariki , alisema wakati wa ujana wake, alikuwa akiona uhusiano unaoboreka kati ya Ufaransa na Ujerumani Magharibi, kupitia kile alichokiita 'pazia la chuma. "Nafurahi kwamba mimi siyo mtazamaji tu, bali ni mtu ambaye nashiriki kikamilifu katika kujenga uhusiano baina ya Ufaransa na Ujerumani," Merkel alimalizia kwa nukuu kutoka kwa De Gaulle, " Udumu urafiki wa Ufaransa na Ujerumani," alisema.

Jenerali Alfred Jodi (kati) akisaini amri ya kujisalimisha kwa wanajeshi wa Ujerumani bila masharti yoyote, iliyowekwa na majeshi ya washirika katika makao makuu ya Kamanda Mkuu Einehowers, mjini Rheims, Mei 7, 1945.
Jenerali Alfred Jodi (kati) akisaini amri ya kujisalimisha kwa wanajeshi wa Ujerumani bila masharti yoyote, iliyowekwa na majeshi ya washirika katika makao makuu ya Kamanda Mkuu Einehowers, mjini Rheims, Mei 7, 1945.Picha: dapd

Sherehe zatiwa dosari na kuharibiwa kwa makaburi ya Wajerumani
Hata hivyo, kumbukumbu hii ya Jumapili ilitiwa dosari kufuatia kuvunjwa kwa mawe yaliyoko kwenye makaburi ya wanajeshi 40 wa Ujerumani, waliopigana vita vikuu vya kwanza vya dunia, yaliyoko kilomita 40 mashariki mwa Rheims.

Uharibifu huu kwenye makaburi ya mtakatifu Etienne-a-Arnes ulilaaniwa vikali na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Manuel Valls. Kwa mujibu wa taarifa, vibao vya msalaba vinavyobainisha makaburi hayo vilichomolewa na vingine kugeuzwa kuni.

Wizara ya mambo ya ndani ilisema uchunguzi unafanyika na njia zote zinachukuliwa kubaini wahusika wa uharibifu huo. Takriban wanajeshi 12,000 wa Ujerumani waliokufa katika vita vya kwanza vya dunia walizikwa katika makaburi hayo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFP, dpa
Mhariri: Mohamed Dahman.