1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Syria mpaka lini?

Admin.WagnerD20 Julai 2012

Shambulizi lililofanyika katika jengo la ulinzi la taifa mjini Damascus ni pigo kubwa kwa mji mkuu huo na kwa uongozi wa Rais Bashar al-Assad, huku wachambuzi wa mambo wakisema huo ni mwisho wa utawala wa Syria.

https://p.dw.com/p/15brM
Mji wa Aleppo nchini Syria.
Mji wa Aleppo nchini Syria.Picha: Reuters

Shambulizi lililofanyika katika jengo la ulinzi la taifa mjini Damascus ni pigo kubwa kwa mji mkuu huo na kwa uongozi wa Rais Bashar al-Assad, huku wachambuzi wa mambo wakisema huo ni mwisho wa utawala wa Syria.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya taifa, waliouwawa katika mkasa huo ni Waziri wa Ulinzi Daoud Rajha, makamu wake Assef Shawkat ambaye pia ni shemeji wa Rais Assad, na naibu makamu wa rais, Hassan Turkmani.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mohammed Ibrahim al-Shaar ni miongoni mwa maofisa wa ngazi ya juu waliojeruhiwa katika mashambulizi hayo, kwa mujibu wa wanaharakati wa upinzani.

Wachambuzi wanasikitishwa na mauaji ya Syria

Mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa Lebanon, Whebe Katisha, amesema mapigano yakifika Damascus na kukaribia makazi ya Rais Assad inamaanisha kwamba mji mkuu huo umeanguka kijeshi.

Rais Basha al- Assad na Waziri Mpya wa Ulinzi Fahd Jassem al-Freij.
Rais Basha al- Assad na Waziri Mpya wa Ulinzi Fahd Jassem al-Freij.Picha: picture-alliance/dpa

Akimuunga mkono Whebe, mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Kimarekani mjini Beirut, Ahmed Mossalli, ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani kuwa siku za utawala wa Syria zimeanza kuhesabika.

Mossali amesema haijulikani ni siku ngapi, miezi mingapi lakini imefikia wakati hata watu wa karibu wa utawala wa Assad wameanza kumpinga.

Mashambulizi hayo ambayo Jeshi Huru la Syria limekiri kulifanya, lilitukia wakati viongozi wa juu wa jeshi na usalama wa taifa walikuwa mkutanoni siku ya Jumatano katika jengo lililopo katika Wilaya ya Rawda.

Mwanzilishi wa jeshi hilo, Riad al- Assad ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani kwa njia ya simu kuwa wanatarajia operesheni hiyo imewachanganya sana watawala wa Syria huku ikiwatia moyo zaidi wanamapinduzi nchini humo.

Ujerumani yasisitiza Urusi na China kubadilisha msimamo

Na hapo jana kabla ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijalipigia kura azimio la kuiwekea vikwazo Syria, Ujerumani kupitia waziri wake wa mambo ya nje, Guido Westerwelle alisema machafuko yanayoendelea Syria hayavumiliki na nchi wanachama wa kudumu wa baraza hilo hawana budi kuungana ili kumaliza machafuko hayo.

Kofi Annan akiteta na Rais wa Urusi, Vladmir Putin.
Kofi Annan akiteta na Rais wa Urusi, Vladmir Putin.Picha: Reuters

Guido Westerwelle alisema: "Jumuia ya kimataifa bado ina fursa ya kuleta suluhisho la kisiasa ili kuzuia mauaji zaidi. Tunatoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa na kwa wanachama wote wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua sasa kuonesha ishara ya wazi ya kupinga umwagikaji damu".

Lakini licha ya ukweli wa wito huo wa Ujerumani, wanachama wawili wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Urusi na China yalitumia kura zao za turufu kulipinga azimio hilo.

Hii ni mara ya tatu katika kipindi cha miezi tisa kuona Urusi na China zikitumia kura hizo kuzuia maazimio muhimu dhidi ya Syria, taifa lililopoteza maisha ya maelfu ya watu katika ghasia zilizodumu kwa miezi 16 iliyopita.

Uingereza imetishwa na maamuzi hayo ya Urusi na China, alisema Balozi wa Uingereza Mark Lyall, ambaye taifa lake ndio lilikuwa mstari wa mbele kuandaa rasimu ya azimio hilo.

Rasimu hiyo inayoungwa mkono na Ujerumani, Marekani, Ufaransa na Ureno inalenga kuiwekea Syria vikwazo ambavyo si vya kijeshi iwapo Rais Bashar al- Assad hataondoa silaha kali katika miji ya Syria katika muda wa siku 10.

Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul\dpa\AFP

Mhariri: Mohammed Khelef