1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel akutana na Wen Jiabao

28 Juni 2011

Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao na Chansela Angela Merkel wa Ujerumani wanakutana leo (28.06.2011) mjini Berlin katika mkutano ambao, pamoja na mengine, unashuhudia kusainiwa kwa mikataba kadhaa ya kibiashara.

https://p.dw.com/p/11kfV
Chansela Angela Merkel (kushoto) na mgeni wake Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, wakikagua gwaride la heshima.
Chansela Angela Merkel (kushoto) na mgeni wake Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, wakikagua gwaride la heshima.Picha: picture alliance/dpa

Asubuhi ya leo, bendi ya jeshi la Ujerumani ilisindikiza gwaride la heshima kwa Waziri Mkuu Wen akiwa na mwenyeji wake, Chansela Merkel, kwenye viwanja vya makao makuu ya serikali ya Ujerumani, mjini Berlin.

Baada ya kukagua gwaride hilo, viongozi wawili hao waliongozana na ujumbe wa mawaziri wao 23, tayari kwa ajili ya mazungumzo yaliyotajwa kuwa ya kiuchumi na kisiasa.

Mikataba ya kibiashara 22 yenye thamani ya euro bilioni 130 inawekwa saini na mataifa haya mawili makubwa kiuchumi duniani.

Hii ni rikodi kubwa kabisa kufikiwa kati ya China inayoshika nafasi ya pili kiuchumi duniani na Ujerumani inayoshikilia nafasi ya nne. Mikataba hii inahusisha biashara ya magari, kemikali na ndege.

Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwenye ziara yake kwenye nchi nyengine za Ulaya, Wen anakabiliwa pia na shinikizo la kisiasa kutoka kwa wenyeji wake kuhusiana na masuala ya haki za binaadamu nchini kwake.

Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao (kushoto) akiwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, jijini London.
Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao (kushoto) akiwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, jijini London.Picha: dapd

Hapo jana, akiwa mjini London, Wen alikwepa kujibu maswali ya waandishi wa habari kuhusiana na mada hii tete, baada ya kuweka saini mkataba wa euro bilioni moja na nusu na mwenzake, David Cameron, wa Uingereza.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema nchi yake haitakuwa laini mbele ya masuala haya ya haki za binaadamu, kwani ni muhimu kwa uhusiano wa kiuchumi.

"Unaosimama hapa ni ushirikiano na raia bilioni moja ambao wanapenda bidhaa zenye kiwango, ambao wanapenda bidhaa kutoka Ujerumani. Na mtu anapotaka kujenga uhusiano nao katika masuala ya kiuchumi, tunapaswa pia kuonesha msimamo wetu katika masuala ya haki za binaadamu na za kiraia. Hapo tutakuwa tunafanya siasa za kweli hasa." Amesema Westerwelle.

Hapo Jumapili (26.06.2011), Ujerumani ilipongeza hatua ya kuachiwa huru kwa mwanaharakati wa China, Hu Jia, ikiwa ni siku chache tu baada msanii na mwanaharakati mwengine, Ai Weiwei, kurudi nyumbani baada ya kushikiliwa na serikali ya China kwa miezi mitatu.

Ujerumani ilikuwa miongoni mwa mataifa ya Magharibi yaliyokuwa yakipigania kuachiwa huru kwa Ai.

Hata hivyo, Ujerumani imeonesha wasiwasi wake juu ya masharti ya kuachiwa kwa wanaharakati hao, ambao wamezuiwa kutokuzungumza na vyombo vya habari.

Wachambuzi wanasema kuachiliwa kwa Ai na Hu kulifanywa katika kipindi hiki cha ziara ya Wen barani Ulaya, ili kuzuia shinikizo la mataifa ya Magharibi kwa China.

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Ujerumani kuzidisha shinikizo lake, kwani linaonekana kufanya kazi.

Wen aliwasili Ujerumani jana, ambapo alikuwa na mazungumzo na jumuiya wa wafanyabiashara wa Ujerumani, akisisitiza umuhimu wa kuheshimiana baina ya mataifa.

"Ni kupitia kuheshimiana baina ya pande mbili tu juu ya tafauti za kiitikadi, ndipo kutakapokuwa na maendeleo kwenye mifumo ya kisiasa na kiuchumi." Alisema Wen.

Baadaye jioni hii, Waziri Mkuu Wen atakutana na Rais wa Ujerumani, Christian Wullf.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman