Merkel aitaka Ulaya ifuate mfano wa Ujerumani | Masuala ya Jamii | DW | 14.06.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Merkel aitaka Ulaya ifuate mfano wa Ujerumani

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ametaka pawepo na mahusiano mazuri ya kijamii kati ya waajiri na waajiriwa, kwani huo ndio msingi wa kuziheshimu na kuzifanya bora zaidi haki za wafanyakazi.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani

Kansela Merkel ameyasema hayo leo jioni (14.06.2011), wakati akihutubia mkutano wa Shirika la Kazi Duniani, ILO, mjini Geneva, nchini Uswisi, ambapo pia alirejea ahadi ya utayarifu wa Ujerumani kuwasaidia kielimu vijana wanaopigania demokrasia katika mataifa ya Afrika ya Kaskazini ili waje wawe na kazi nzuri.

Hapana shaka, ujumbe wa Kansela Merkel umepokelewa vyema na washiriki wa mkutano huu, kwani hata kabla hajapanda kutoa hotuba yake, kulikuwa na shamrashamra nyingi za kumkaribisha kutoka viongozi kadhaa wanaowakilisha serikali zao kwenye mkutano huu wa kimataifa.

Na kubwa hasa ambalo limempatia heshima hii Kansela Merkel ni namna ambavyo nchi yake imejikaza kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi na kifedha, ambao umekuwa ukiyakumba mataifa mengi ya Ulaya.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Juan Somavia

Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Juan Somavia

Kansela Merkel ameyataka mataifa mengine yaige mfano wa Ujerumani kwenye utendaji na usimamizi wa kazi, ambao amesema umejengeka juu ya mahusiano mema kati ya waajiri, waajiriwa na serikali.

"Somo la ulimwengu kujifunza kutokana na mgogoro huu ni kwamba lazima pawe na mahusiano zaidi ya kijamii, kama ilivyo wakati wa kufanya maamuzi ya uwekezaji, ndivyo pia iwe wakati wa mgogoro. Lazima pawepo na ushirikiano mkubwa." Amesema Kansela Merkel.

Kansela Merkel hakuishia kwenye suala la hali ya mazingira ya kazi tu barani Ulaya, bali pia katika wimbi la mageuzi kwenye ulimwengu wa Kiarabu, ambako watu wanaendelea kumiminika mitaani kupigania demokrasia na uhuru zaidi.

Amethibitisha tena kwamba Ujerumani iko tayari kuyasaidia mataifa ya Kaskazini mwa Afrika na Arabuni, kwani ni sehemu kubwa ya watu kwenye jamii hizo ni vijana ambao lazima wasaidiwe kielimu, kusudi waje wawe na kazi nzuri.

Waziri wa Nje wa Marekani, Hillary Clinton (kushoto) na Kansela Angela Merkel

Waziri wa Nje wa Marekani, Hillary Clinton (kushoto) na Kansela Angela Merkel

"Kwa hiyo katika mchakato huu Ujerumani inataka kuja na kitu, kwamba tuanzishe aina fulani ya mkataba wa shughuli ambao utaowawezesha vijana wengi kupata elimu, ili wawe na sifa zitakazowawezesha kupata kazi nzuri katika nchi zao, ili kuuendeleza mchakato wa kuziimarisha taasisi za kijamii ndani ya jamii zao." Amesema Kansela Merkel.

Mpango huu aliuotaja Kansela Merkel ni ule unaoungwa mkono pia na Ufaransa, na ambao mataifa haya mawili yaliupendekeza kwenye mkutano wa mwezi uliopita wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda, G20, uliofanyika huko Deuaville, Ufaransa.

Kansela Merkel amesisitiza kwamba ni muhimu kuzitia vitendoni zile ahadi zilizotolewa na mataifa ya G20 kwa kuwashirikisha wahusika wenyewe.

"Lazima tuhakikishe kuwa mijadala hii ya G20 haiwi mijadala tu ya maneno kuhusu masuala ya fedha, lakini la muhimu zaidi ni kwamba watu wote duniani wanafahamu kwamba lengo ni nini na wanaelekea wapi."

Kansela Merkel pia amesema pia kwamba Ujerumani inataka kuwa na jukumu maalum katika Umoja wa Mataifa, Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD, na pia kwenye Shirika la Kazi la Ulimwengu, ILO.

"Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Umoja wa Mataifa ulijishughulisha zaidi na masuala ya amani na usalama wa ulimwengu tu, na sasa kuna masuala ya mashirikiano ya kimataifa na maendeleo ya kiuchumi, ambayo sisi tunataka tuwe sehemu yake muhimu." Amesema Kansela Merkel.

Baadaye Jumatano (15.06.2011), Kansela Merkel anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa Urusi, Vladimir Putin. na Waziri wa Mambo wa Nje wa Uswisi, Micheline Calmy-Rey.

Mwandishi: Malte Pieper/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

 • Tarehe 14.06.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11aBc
 • Tarehe 14.06.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11aBc

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com