1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ziarani Marekani

7 Juni 2011

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amewasili mjini Washington Marekani, kwa ziara ya siku mbili. Amesisitiza umuhimu wa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

https://p.dw.com/p/11Vas
Rais wa Marekani, Barack Obama (kushoto) na kansela wa Ujerumani Angela Merkel (wa pili kushoto) wakiondoka mkahawa wa 1789 Georgetown, WashingtonPicha: picture alliance/dpa

Baada ya kuwasili nchini humo jana jioni, Kansela Angela Merkel alilakiwa na mwenyeji wake Rais Barack Obama ambaye alimkaribisha kwa chakula cha jioni kwenye mkahawa wa 1789 mjini Washington. Duru za serikali ya Ujerumani zimeeleza kuwa katika mkutano wao huo wa kwanza baada ya kuwasili, Rais Obama na Kansela Merkel walizungumzia masuala kuhusu operesheni za Jumuiya ya Kujihami ya NATO Afrika Kaskazini na Afghanistan, mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati na mzozo wa sarafu ya Euro. Kwa mujibu wa duru hizo, mazungumzo hayo yalikuwa ya mafanikio makubwa na kwamba viongozi hao pia walibadilishana maoni ya kirafiki.

Akizungumzia upendo wake alionao kwa Ujerumani, Rais Obama alisema, "Daima nimekuwa na moyo mkunjufu na Ujerumani. Nitawaeleza kwamba sehemu ya moyo huo nahisi ni kwa sababu nampenda sana Kansela Merkel. Merkel ni madhubuti, mtendaji na anaposema kitu ninamuamini."

Hata hivyo, hapakuwa na taarifa zozote kuhusu tofauti baina ya nchi hizo mbili katika suala la Libya. Mwezi Machi mwaka huu, Ujerumani haikulipigia kura azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kuweka marufuku ya ndege kuruka katika anga ya Libya, huku Marekani ikipiga kura kuliunga mkono azimio hilo ambapo pamoja na washirika wake wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO zinaendesha mashambulio ya anga dhidi ya utawala wa Kanali Muammar Gaddafi.

Rais Obama na Kansela Merkel wamekuwa hawafichi tofauti zao katika makubaliano mbalimbali kama suala la matumizi ya fedha za serikali wakati wa mzozo wa kiuchumi, ambapo Rais Obama alitaka serikali kuchangia zaidi katika kuinua uchumi, huku Kansela Merkel akishinikiza hatua kali za kubana matumizi. Viongozi hao watajadiliana pia mzozo wa madeni katika kundi la mataifa yanayotumia sarafu ya Euro. Lakini wakati Ugiriki imeanza kampeni ya kupata msaada mpya wa kimataifa, utawala wa Rais Obama umeweka wazi kuwa inatarajia Ulaya na hasa Ujerumani kulishughulikia tatizo hilo.

Akijibu swali iwapo Marekani itaunga mkono utoaji wa fedha zaidi kwa Ugiriki kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jay Carney alisema Ulaya ina njia za kuisaidia Ugiriki peke yake. Marekani pia inakabiliwa na changamoto ya deni na Kansela Merkel anaweza kukataa wazi wazi wito wa Obama kuhusu Ugiriki kwa kusema Marekani lazima itatue yenyewe matatizo yake ya kifedha.

Ziara ya Kansela Merkel inaanza rasmi leo ambapo atapigiwa mizinga 19 wakati wa sherehe rasmi za kukaribishwa katika Ikulu ya Marekani. Kansela Merkel pia atatunukiwa na Rais Obama, medali ya uhuru inayotolewa na rais wa Marekani, tuzo ya juu kabisa ya kiraia na kumuandalia rasmi chakula cha jioni. Kansela Merkel ameongozana na mawaziri wake watano idadi inayoelezwa kuwa kubwa zaidi katika ujumbe wa ngazi ya juu ya Ujerumani tangu utawala wa Kansela Helmut Kohl.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE,RTRE)

Mhariri:Hamidou Oummilkheir